Saturday, May 22, 2010
Mkongwe Sol Campbell aweweseka kutoitwa England
Mkongwe Sol Campbell aweweseka kutoitwa England
LONDON,England
BEKI wa Arsenal, Sol Campbell amesema kuwa amefadhaika baada ya kocha Fabio Capello kutompatia nafasi katika kikosi cha timu ya Taifa ya England kitakachokwenda kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Msimu huu mkongwe huyo alianza kwa kuichezea timu ya ligi daraja la pili Notts County kabla ya kuhamia Gunners wakati wa usajili wa dirisha la majira ya baridi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 baada ya kurejea Ligi Kuu na kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya alionesha cheche zake na kocha wa Gunners, Arsene Wenger anaamni kuwa anastahili kwenda kucheza kwenye fainali hizo.
Kwa upande wake Campbell ambaye ni nahodha wa zamani wa England anaamini kuwa kwa kucheza kwake Arsenal na uwezo wake anapaswa kuwemo katika kikosi cha kocha Capello ambacho kitaelekea Afrika Kusini wiki chache zijazo.
“Hata kama kiwango changu kuwa juu mwishoni mwa msimu haijalishi kwani bado niko fiti ikilinganishwa na wachezaji wengi ambao wamechoka baada ya kucheza muda mrefu,” Campbell aliliambia gazeti la Daily Star.
“Sijawahi kukutana na Capello, lakini unaweza kubaini kuwa haniitaji kama mchezaji kwa sababu hajawahi kunifikiria,”aliongeza.
Alisema kutoitwa kwake siyo kwa sababu ya umri kwani kocha huyo kwa sasa anajaribu kuwashawishi wachezaji kama Paul Scholes na Jamie Carragher,"waendelee kuichezea timu hiyo.
Katika kipindi ambacho alikuwa akiichezea England Campbell alionekana uwanjani mara 73 huku akiwaameichezea timu hiyo mara tatu katika fainali za Kombe la Dunia.
Mara ya mwisho beki huyo kuichezea England ilikuwa ni katika mechi ambayo timu hiyo ilichapwa mabao 3-2 na Croatia iliyopigwa kwenye uwanja wa Wembley Novemba 2007 kichapo ambacho kilimgharimu kibarua cha aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Steve McClaren kushindwa kwenda fainali za Mataifa ya Ulaya.
,
No comments:
Post a Comment