Wednesday, June 9, 2010

POLISI WAVYATUA RISASI RUGWE WAKATI WA OPERESHENI YA KUKAMATA WAFANYABIHASHARA WASIOLIPA HUSHURU

Na Thobias Mwanakatwe,Tukuyu

VURUGU kubwa zilizowalazimu polisi kufyatua risasi za moto katika kijiji cha Mpuguso wilayani Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa operesheni ya kukamata wafanyabiashara wasiolipa ushuru wa soko na wale wasiokuwa na leseni za biashara zimesababisha mamia ya wananchi kuzihama nyumba zao na kukimbilia vijiji vya jirani.

Tukio hilo limetokea juzi Jumapili baada ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kuwatumia polisi pamoja na mgambo kuendesha operesheni ya kuwakamata wafanyabiashara sugu ambao wamekuwa wakikaidi kulipa ushuru wa soko na wengine wakiendesha biashara za maduka bila kuwa na leseni kinyume cha taratibu na sheria za biashara.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mpuguso,Seif Seleman akizungumza na Nipashe jana alisema kutokana na vurugu hizo wananchi wake walilazimika kukimbilia vijiji jirani vya Isajilo, Pumbuli,Ibula na Katonya kujinusuru kufutia polisi na mgambo kufyatua risasi ovyo.

Seleman alisema polisi na mgambo walifika kwa kushtukiza katika kijiji hicho juzi wakiwa wameambatana na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe na kuanza kuwakamata watu wanaokaidi kulipia ushuru na leseni za biashara na ndipo kulitokea vurugu za wananchi waliokuwa wakipinga kitendo hicho na hivyo kuwalazimu polisi kufyatua risasi hewani.

“Mkrugenzi wa Halmashauri alikuja na polisi pamoja na mgambo na kuanza kuendesha operesheni ya kuwakamata watu ovyo hapa kijiji ndipo kukatokea vurugu na polisi wakafyatua risasi tatu hewani kutawanya wananchi waliokuwa na jazba”alisema Seleman.

Mwenyekiti huyo alisema katika vurugu hizo ambazo hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa, wafanyabiashara kadhaa wa kijiji hicho wamenyang’anywa bidhaa mbalimbali za dukani kama vile magodoro,mafuta ya kupikia na kupaka,ndizi na nguo ambavyo vimepelekwa wilayani.

Alisema kinachowashangaza wananchi ni kuendeshwa kwa operesheni hiyo kwa kutumia nguvu sana na kuwashtukiza ambapo uongozi wa serikali ya kijiji hicho haikupewa taarifa za kuwepo kwa zoezi hilo hali inayotia mashaka kuwa huenda kuna ajenda ya siri na hasa ikizingatiwa kuwa uongozi wa kijiji hicho ni wa chama cha upinzani cha Chadema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Emmanuel Mahyenga, akizungumza na Nipashe kwa simu alisema hawezi kueleza kwa undani tukio hilo kwasababu yupo njiani kuelekea Moshi kuhudhuria mkutano wa ALAT na kuahidi kulitolea maelezo mara atakapofika.

Kwaupande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe,Jackison Msome, alisema taarifa za kuwepo kwa vurugu hizo amezipata na kwamba ofisi yake inaendelea kulifuatilia.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alisema kweli tukio hilo limetokea na kwamba hata hivyo katika operesheni kama hizo polisi waga wanaobwa tu na halmashauri husika ili kunapotokea vurugu kusitokee uvunifu wa amani.

No comments:

Post a Comment