Wednesday, June 9, 2010
WANACHAMA WANNE WA CCM KUGOMBEA JIMBO LA KWELA
Dr Harrison George MBUGE CCM
Na Thobias Mwanakatwe, Sumbawanga
BAADA ya Mbunge wa jimbo la Kwela Sumbawanga Vijijini, Dk.Chrisant Mzindakaya, kutangaza kwamba hana mpango wa kugombea ubunge mwaka huu, wanachama wanne wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuwania nafasi hiyo akiwemo Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji kilichopo jijiji Mbeya, Stephen Chambanenge.
Chambanenge ambaye yupo kwenye kitivo cha Sayansi ya Jamii katika chuo hicho,akizungumza na Nipashe jana alisema ameamua kugombea ili kuleta changamoto mpya ya maendeleo katika jimbo hilo ambalo linakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo ubovu wa miundombinu hususani ya barabara.
“Ubunge wa sasa unahitaji mtazamo mpya unaoshabihiana na kasi ya karne ya Sayansi na Teknolojia hivyo maarifa ya kisasa na uwezo wa kufikiri na kutenda kwa haraka kunahitajika ili kuleta kasi ya maendeleo,”alisema Chambanenge.
Alisema jimbo la Kwela ambalo asilimia zaidi 80 ya wakazi wake ni wakulima bado linakabiliwa na matatizo kadhaa kama vile ukosefu wa soko la uhakika la kuuzia mazao yao na hivyo wafanyabiashara wakubwa kuwalangua kwa kununua mazao kwa bei ndogo na kusababisha wakulima kuendelea kuwa maskini.
Chambanenge alisema kama Chama cha Mapinduzi kitamteua kuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo na wananchi kumchagua kipaumbele chake cha kwanza itakuwa ni kuinua hali ya maisha ya kipato cha wananchi kwa kuboresha upatikanaji wa soko la mazao na kuifanya ardhi itumike kama rasmali ya kutoamitaji kwa wananchi.
Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mariamu Mwambanga, akizungumza na Nipashe kwa simu jana aliwataja wanachama wengine waliotangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Kwela kuwa ni pamoja na Diwani wa kata ya Milepa, Ignas Malocha.
Wengine ni Afisa Elimu Vifaa na Takwimu Wilaya ya Kasuru mkoani Kigoma, Benedict Chapewa na Meja Jenerali Januari Kisanko.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Sumbawanga vijiji walioongea na gazeti hili walisema DkMzindakaya ambaye amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 30 amesoma alama za nyakati ndiyo maana ameamua kutangaza hadharani kuwa hana tena mpango wa kugombea nafasi hiyo ya ubunge.
Walisema kwa vyeo ambavyo amewahi kushika katika nchi hii, inatosha kusema Dk. Mzindakaya anastaafu siasa akiwa na heshima nyingi za utumishi kwa wananchi wake na kwa Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment