Thursday, June 7, 2012

TBL:TUNA IMANI NA TIMU YA TAIFA,KOCHA


 Yataka timu iwekaribu na wananchi
Kavishe akisalimia wachezaji wa timu ya Stars leo jijini Dar es Salaam
NA MWANDISHI WETU
Kampuni ya Bia Tanzania ambayo ni mdhamini mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager imesema ina imani na timu hii na kocha wake na kuahidi kuedelea kuipa nguvu ili ifanikiwe zaidi.
     Hayo yamesemwa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wakati akitambulishwa rasmi kwa Timu ya Taifa na Nahodha wa Timu hiyo JUma Kaseja na Kocha Kim Poulsen na kupata chakula cha mchana na wachezaji.
     Bwana Kavishe aliwapongeza kwa kujitahidi wakati wa mechi yao na Ivory Coast Jumamosi iliyopita. “Nimeelezwa kuwa mlicheza vizuri kwa kujituma na tulikosa nafasi nyingi za kufunga magoli,” alisema Bwana Kavishe.
     Alisema kampuni yake inaamini huu ni mwanzo tu na timu ina nafasi ya kupata matokeo mazuri zaidi katika mechi zijazo hasa hii ya Jumapili dhidi ya Gambia ya mchujo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia.
     “Lazima tuwafanye watanzania wajione kama sehemu ya timu ya taifa ili watushangilie wakati tunacheza ili ifike wakati walie na sisi tunapolia na wacheke na sisi tunapocheka,” alisema na kuongeza kuwa amefurahishwa na kocha wa Timu ya Tifa alivyo na ari ya kuendeleza soka la Tanzania na matumaini anayowapa wachezaji.
    Aliwaasa wachezaji wawe karibu na wananchi ili waweze kujiskia kama sehemu ya Timu ya Taifa na kuongeza kuwa watanzania wana matumainai makubwa na timu yao kwa hivyo ni jukumu la wachezaji kuendelea kuwapa matumaini na kujituma uwanjani.
    Bwana Kavishe alisema amefurahishwa na jinsi kocha wa sasa ameweka nidhamu katika timu ya taifa kwani ni jambo muhimu kwa mchezaji wowote.
     Naye kocha wa Timu ya Taifa Kim Poulsen aliishukuru Kampuni ya Bia Tanzania kwa udhamini wake mnono kupitia kinywaji chake cha Kilimanajro Premium Lager na kuongeza uwa timu haiwezi kuwa imara bila udhamini wa uhakika.
    “Kwa sasa tunaweza kufanya mipango ya muda mrefu bila wasiwasi wowote kwa sababu udhamini ni wa uhakika,” alisema.
    Poulsen alisema amefurahishwa sana na udhamini wa Timu ya Taifa na kwamba viwango vya wachezaji vinazidi kuimarika siku hadi siku.
     Mpaka sasa Timu ya Taifa imecheza mechi mbili tangu itangazwe rasmi ya kwanza ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Malawi ambapo timu zote mbili zilitoka sare ya bila kufungana na mechi ya pili ilikuwa dhidi ya Ivory Coast ambayo ilikuwa mchujo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia ambapo Stars ilifungwa 2-0.
    Jumapili hii Stars inatarajiwa kucheza na Gambia katika mchujo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia.

No comments:

Post a Comment