Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa
masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Mara (FAM), Fabian Samo kilichotokea leo asubuhi (Julai 10 mwaka huu).
Samo ambaye Novemba 13 mwaka jana alichaguliwa kwa kipindi
cha pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa FAM katika uchaguzi uliofanyika wilayani
Rorya alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam
akisumbuliwa na maradhi ya figo.
Taratibu za mazishi ya Samo ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati
ya Ukaguzi wa Hesabu (Internal Audit Committee) ya TFF ikiwemo siku
atakayozikwa bado zinafanywa na familia yake.
Samo alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mpira wa
miguu mkoani Mara na Tanzania
kwa ujumla, vitu ambavyo vilichangia kuchaguliwa kwake tena kuiongoza FAM.
Msiba huo ni pigo kwa familia ya Samo, FAM, TFF na mchezo wa
mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango na mawazo aliyotoa kwa
kipindi chote alichokuwa kiongozi.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Samo, FAM, jamaa na
marafiki na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.
Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama
rambirambi zake.
No comments:
Post a Comment