Friday, August 17, 2012

LIGI KUU YA ENGLAND KUANZA KUPIGWA KESHO


LONDON, England
MBIO ndefu za kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu ya England zinaanza rasmi kesho, ambapo klabu 14 kati ya 20 za ligi hiyo zitajitupa kwenye viwanja mbalimbali, kuwania pointi tatu muhimu katika siku hii ya ufunguzi.
Pazia la ligi hiyo lililofunguliwa wiki jana kwa pambano la Ngao ya Jamii baina ya mabingwa watetezi Manchester City na mabingwa wa Kombe la FA, Chelsea, litashuhudia muendelezo wake hapo kesho-kutwa Jumapili na Jumatatu usiku.

Klabu iliyoipa Man City ubingwa katika dakika za mwisho za siku ya kuhitimisha ligi msimu uliopita QPR, itakuwa nyumbani kuumana na Swansea, huku Reading iliyorejea Ligi Kuu ikishuka kwenye uwanja wa nyumbani kuwaalika Stoke City.

Washika Bunduki walio kwenye sikitiko la kumpoteza mkali wake Robin Van Persie, wanaanzia nyumbani Emirates kesho, kwa kuwaalika Sunderland, huku Wekundu wa Anfield Liverpool wakisafiri kuwafuata West Brom.

Wagonga Nyundo wa London, West Ham United, wataumana na Aston Villa, huku Fulham ikitarajiwa kushuka kwenye dimba la Craven Cottage kupimana na ubavu na Norwich City, mechi zote hizo zinatarajiwa kuchezwa saa 9:00 alasiri (sawa na saa 11 jioni kwa Afrika Mashariki).

Pambano linalotazamwa na wengi hapo kesho litapigwa 11:30 (sawa na saa 1:30 Afrika Mashariki), ambapo Newcastle United watakapowakaribisha Tottenham – inayonolewa na kocha Andre Villas-Boas.

Jumapili watetezi Man City wanatarajia kutupa karata yao kwanza hapo kwa kuumana na Southampton kwenye Uwanja wa Etihad, huku Wigan ikiwa nyumbani kuwapima wabingwa wa FA waliolala katika Ngao ya Jamii, Chelsea.

Mechi za ufunguzi wa ligi hiyo zitahitimishwa Jumatatu usiku, wakati Manchester United watakapoumana na Everton pambano linalotarajiwa kuwa la kwanza kwa Mholanzi Van Persie, aliyekamilisha uhamisho wa kuchezea United akitokea Gunners.

No comments:

Post a Comment