Friday, August 17, 2012

SNEIJDER: KUFUNGWA UHOLANZI WALAUMIWE DE JONG, STEKELENBURG


Kiungo wa Uholanzi, Nigel de Jong kushoto akichuana na mshambuliaji wa Ubelgiji

AMSTERDAM, Uholanzi

NAHODHA mpya wa timu ya taifa ya Uholanzi, Wesley Sneijder, ameshindwa kujizuia na kuwataja Nigel de Jong na Maarten kama waliochangia kufungwa mabao 4-2 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ubelgiji kwenye Uwanja wa Roi Baudouin.

Sneijder aliyetangazwa siku moja kabla ya mechi na kocha Louis van Gaal kurithi unahodha ulioachwa na Mark van Bommel aliyestaafu soka, amesema ni kweli ‘walipoteana’ kipindi cha kwanza, lakini makosa ya kizembe ya nyota hao yaliwaponza hata waliporejea mchezoni kipindi cha pili.

“Ni kweli hatukucheza vema kwa dakika 45 za kwanza. Lakini tulikuwa bora zaidi dimbani katika kipindi cha pili, lakini lazima niseme kwamba tumeponzwa na makosa binafsi ya kiungo Nigel de Jong na mlinda mlango Maarten Stekelenburg,” Sneijder aliwaambia waandishi wa habari wa Uholanzi.

Mkali huyo aliyecheza mechi ya 87 akiwa na jezi za taifa za Uholanzi, aliumwagia sifa mfumo bora wa ufundishaji na upangaji kikosi wa kocha wake Louis van Gaal, licha ya kujikuta wakiangukia pua katika mechi hiyo.

“Nadhani mfumo mpya wa kocha umeifanya timu kuwa bora na imara kimchezo na kimbinu (akiuzungumzia mfumo wa 4-3-3 badala ya ule wa 4-2-3-1 ulioiponza timu kwenye mashindano ya Euro 2012).

“Tulikuwa na nafasi nyingi za kufunga ambazo hatukuzitumia, lakini kimsingi tulicheza vema kwa muda fulani,” alihitimisha Sneijder.

Ubelgiji waliokuwa nyumbani, walimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa mbele kwa bao la Christian Benteke, ambapo kipindi cha pili Uholanzi ikasawazisha kwa bao Luciano Narsingh dakika ya 54, kabla ya Klaas-Jan Huntelaar kufunga la uongozi kwa Oranje.

Ndipo De Jong alipotoa ‘boko’ kwa Dries Mertens, ambaye alijivuta kwa kasi kuingia ndani ya boksi na kufumua shuti kuisawazishia Ubelgiji, kabla ya Romelu Lukaku kuifungia bao la tatu. Kipa wa Uholanzi, akafanya kosa lililozaa bao la nne na kumfanya Sneijder afure kwa hasira.

No comments:

Post a Comment