Saturday, August 25, 2012

ZAO LA TWANGA PEPETA 2006!









ASILI yake ni huko mkoani Tanga yalikozaliwa mapenzi! Anatokea kwenye kabila wa Wabondei. Jina lake lilianza kukua kupitia ulimwengu wa habari. Alikuwa mtangazaji akapitia katika Shindano la Kimwana Manywele Twanga Pepeta 2006/07 na sasa anafurukuta zaidi katika ulimwengu wa filamu za Kibongo.
Anaitwa Lulu Mathias Semagongo ‘Aunt Lulu’. Amezaliwa mwaka 1987 jijini Dar. Mwaka 1993 alijiunga na Shule ya Msingi ya Kumbukumbu ya Dar na kufanikiwa kumaliza masomo mwaka 1999.


Mwaka 2000, Aunt Lulu alijiunga na Shule ya Sekondari ya Kisutu hadi alipohitimu mwaka 2004.
UTANGAZAJI
Kipaji kwa Aunt Lulu kilijionesha waziwazi tangu akiwa shule ya msingi. Mwaka 1998 hadi 2003 alikuwa akitangaza kipindi cha watoto cha Redio One na ITV kilichojulikana kwa jina la Watoto Show.
Mwaka 2004 hadi 2006, mkali huyo aliyeonesha cheche katika kutumia kipaza sauti, alihamia Redio Magic FM ya jijini Dar. Akiwa hapo alitangaza kipindi kilichofahamika kama Ulingo wa Watoto, wakati huohuo akiwa kwenye mtandao wa vijana uliokuwa ukijishughulisha na matatizo yanayowakabili watoto chini ya mfuko wa shirika linalojishughulisha na haki za watoto duniani la UNICEF.


KIMWANA WA TWANGA PEPETA.
Mwenye kipaji siku zote siyo mwenzako, mwaka 2006, Aunt Lulu alijitosa kwenye Shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta lililokuwa likitafuta mnenguaji bora. Aunt Lulu alijishindia taji hilo na kunyakuwa zawadi ya gari.


Mara baada ya kuongezeka jina lake kupitia Kimwana Manywele, Aunt Lulu alitumia nafasi hiyo kusoma kozi fupi za kompyuta kabla ya kujiunga na kampuni ya Bench Mark Production mwaka 2007.


“Bench Mark Production nilikuwa kama Assistant Producer, pia nilikuwa host wa kipindi cha Wimbo kilichorushwa kupitia ITV,” anasema.

ARUDI DARASANI
Mwaka 2008, mtangazaji huyo alirudi darasani akasomea kozi ya Kingereza pale British Council, Dar na kufanikiwa kuhitimu masomo hayo katika ngazi ya cheti (advance certificate).

SKENDO
Maisha ya Aunt Lulu yaliendelea kushamiri katika kazi ingawa pia aligubikwa na skendo za hapa na pale kama ulevi wa kupindukia na mengine mengi yanayofanana na hayo. Mara kakutwa amelewa klabu, mara kanaswa sehemu na mwanaume na mengineyo.

UTANGAZAJI TENA
Mwaka 2009 hadi 2011, Aunt Lulu mwenye matukio kibao mjini, alipata nafasi ya kutangaza katika Televisheni ya C2C. Aliposimama kutangaza mwaka 2011, aliamua kuingia kwenye darasa lihusulo taaluma yake ya utangazaji. Akajiunga na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) kilichopo Makumbusho jijini Dar na kufanikiwa kupata cheti.

FILAMU
Mwaka 2012, Aunt Lulu amekuja kivingine baada ya kugundua ana kipaji cha uigizaji. Kwa kukubali ushauri aliopewa na mpenzi wake (Bond Bin Salim), akaanza kuigiza chini ya Kampuni ya Richard Dyle Bezuidenhout (Richard wa BBA).

ANAFANYA NINI KWA SASA?
Mpaka leo, Aunt Lulu bado anafanya shughuli za U-MC katika sherehe mbalimbali huku akiwa ameelekeza nguvu zake katika ulimwengu wa filamu za Kibongo.



MAFANIKIO
Mwenyewe anasema mafanikio makubwa zaidi ni kujulikana, ukiacha kiwanja chake alichonunua ambacho bado hajaanza ujenzi.






No comments:

Post a Comment