Monday, October 15, 2012

MINTANGA AACHIWA BAADA YA KUSOTA RUMANDE MIAKA 4, HAKUWAHI KUSIKILIZWA HATA SIKU MOJA.


MAHAKAMA Kuu Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo imemwachia huru Rais wa zamani wa Chama cha Ngumi za Ridhaa nchini (BFT), Alhaj Shaaban Mintanga aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la  kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa Kilo 4.8 kutoka Tanzania kwenda Mauritius baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo.
Akitoa hukumu hiyo leo, Jaji wa Mahakama hiyo, Twalib Fauz, alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo hivyo kumuachia huru mshitakiwa huyo.
Mintanga alikamatwa Aprili 4, 2008 nchini Mauritius ambako alikwenda na Timu ya Taifa Ngumi za Ridhaa akiwa kiongozi.  Mara baada ya kukamatwa na madawa hayo alishitakiwa na kurejeshwa nchini ambako alifunguliwa kesi iliyodumu kwa muda wa miaka minne ambapo ameachiwa huru leo.
Katika kipindi chote cha kesi hii haikuwahi kusikilizwa hata mara moja zaidi ya kuahirishwa kila ilipotajwa, hali iliyofanya mtuhumiwa kudhoofika kiafya kutokana na hali aliyokuwa nayo huko gerezani.  Mwenendo wa kesi hiyo uliwafanya baadhi ya wadau kuona kama kulikuwa na mkono wa mtu wenye lengo la kumkomoa.
Mintanga ambaye ni muumini mzuri wa dini ya Kiislamu aliyewahi kwenda kuhiji Maka mara baada ya hukumu hiyo ya kuachiwa huru, alionekana kutabasamu na hakupenda kuzungumza chochote na vyombo vya habari bali alikwenda kwenye moja ya vyumba vya mahakama na kukaa huko.
Mpaka mtandao huu unaondoka mahakamani, Mintanga alikuwa hajaondoka katika chumba hicho.

No comments:

Post a Comment