Na Anna Nkinda – Maelezo, New York
Ilielezwa
kwamba ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake katika jamii hakutakuwa na
mtoto atakayekosa elimu kwa ajili ya kutokuwa na ada, vitabu na nguo za
shule pia hakutakuwa na watu watakaokufa kwa kukosa chakula na malazi.
Ili
kuhakikisha hayo yote yanafanikiwa jitihada za pamoja zinahitajika kwa
wadau wote wa maendeleo kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana ili
waweze kutimiza malengo na mipango waliyojiwekea.
Hayo
yasemwa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwasilisha mada
kuhusu uvumilivu na uongozi wa wanawake wa Afrika katika kukabiliana na
changamoto za kibinadamu kwenye mkutano maalum wa kujadili utekelezaji
wa huduma za kibinadamu barani Afrika uliofanyika mjini New York nchini
Marekani.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema kupatikana kwa elimu bora kwa mtoto kutamwezesha kupata
fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya bora, kuongezeka kwa kipato cha
familia na hivyo kujikwamua na hali ya umaskini.
“Kitaaluma
mimi ni mwalimu nafahamu changamoto zinazowakabili watoto na familia
zao wakati wanajitahidi kupambana na ujinga, magonjwa na maisha ya
umaskini kutokana na hali hii, mimi naona kuwapatia elimu ni njia moja
wapo itakayowafanya waweze kuepukana na umaskini kwani mara wamalizapo
masomo yao wataweza kupata ajira na hivyo kujitegeme”, alisema Mama
Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huo kuwa aliamua
kuanzisha taasisi hiyo ambayo kupitia kwake ameweza kuhakikisha watoto
wa kike wanakwenda shule kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kusoma kwani
mtoto wa kike akikaa shule muda mrefu ndivyo anavyoweza kuepukana na
mimba za utotoni, vifo wakati wa kujifungua na hali ya umaskini.
Mama
Kikwete alisema, “kutokana na hali hii tumejenga shule ya sekondari ya
mfano ya WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo
inatoa elimu bure kwa watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika
mazingira hatarishi nia ya kuanzisha shule hii yenye wanafunzi wa
kidato cha kwanza hadi cha nne 325 ni kuwapatia watoto hawa elimu sawa
na wenzao ambao wanawazazi.
Kazi
nyingine zinazofanywa na Taasisi hiyo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi
kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwaongezea mitaji ya
biashara na kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo wanatarajia kuwafikia
wanawake 60000.
Pia
wanahakikisha vifo vya kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa
chini ya miaka mitano vinapungua kwa kutoa elimu kwa jamii jinsi gani
inaweza kuepukana na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto na kutoa elimu ya jinsia na uzazi kwa vijana ili
waweze kuepukana na mimba za utotoni na ugonjwa wa Ukimwi.
Akifungua
mkutano huo Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
anayeshughulikia unyanyasaji wa kijinsia na utatuzi wa migogoro Zainabu
Bangura alieleza kwamba katika bara la Afrika wanawake wanazalisha mali
kwa asilimia 70 ya uchumi usio rasmi na asilimia 20 kwa uchumi rasmi
hivyo basi kuwanyanyasa, kuwabagua, kuwakandamiza na kuwadidimiza
wanawake ni sawa na kudidimiza taifa zima.
Msemaji
Mkuu katika mkutano huo kutoka Umoja wa Afrika (AU) Aisha Abdullahi
ambaye ni Kamishina anayeshughulikia masuala ya siasa alisema kuwa
pamoja na ukweli kwamba ndani ya Bara la Afrika kuna utashi mkubwa wa
kisiasa na nia ya kushughulikia changamaoto za masuala ya kibinadamu,
bado bara hilo linakabiliwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani na nje
zaidi ya million 15.
Abdhullahi
alisema, “Wakimbizi hawa wanahangaika kutafuta mavazi, chakula na
makazi maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika. Pamoja na changamoto
nyingine za umaskini, uchumi duni na matatizo ya kisiasa katika baadhi
ya nchi Umoja wa Afrika umeliweka suala la wakimbizi kuwa ni moja
ya agenda zake muhimu”.
Mkutano
huo ulioandaliwa na ofisi za umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya
kibinadamu (OCHA) na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka ofisi za
taasisi za kimataifa na kikanda.
No comments:
Post a Comment