Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, September 27, 2013

JAMII YATAKIWA KUWASAIDIA WATOTO ILI WAWEZE KUPATA ELIMU


Na Anna Nkinda – Maelezo, New York

Ilielezwa kwamba ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake katika jamii hakutakuwa na mtoto atakayekosa elimu kwa ajili ya kutokuwa na ada, vitabu na nguo za shule pia hakutakuwa na watu watakaokufa kwa kukosa  chakula na malazi.
Ili kuhakikisha hayo yote yanafanikiwa jitihada za pamoja zinahitajika kwa wadau wote wa maendeleo  kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana ili waweze kutimiza malengo na mipango waliyojiwekea.
Hayo yasemwa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwasilisha mada kuhusu uvumilivu na uongozi wa wanawake wa Afrika katika kukabiliana na changamoto za kibinadamu kwenye mkutano maalum wa kujadili utekelezaji wa huduma za kibinadamu barani Afrika uliofanyika mjini New York nchini Marekani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kupatikana kwa elimu bora kwa mtoto kutamwezesha  kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya bora, kuongezeka kwa kipato cha familia na hivyo kujikwamua na  hali ya umaskini.
“Kitaaluma mimi ni mwalimu nafahamu changamoto zinazowakabili watoto na familia zao wakati wanajitahidi kupambana na ujinga, magonjwa na maisha ya umaskini  kutokana na hali hii, mimi naona kuwapatia elimu ni njia moja wapo itakayowafanya waweze kuepukana na umaskini kwani mara wamalizapo masomo yao wataweza kupata ajira na hivyo kujitegeme”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huo kuwa aliamua kuanzisha taasisi hiyo ambayo kupitia kwake ameweza kuhakikisha watoto wa kike wanakwenda shule kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kusoma kwani mtoto wa kike akikaa shule muda mrefu ndivyo anavyoweza kuepukana na mimba za utotoni, vifo wakati wa kujifungua na hali ya umaskini.
Mama Kikwete alisema, “kutokana na hali hii tumejenga shule ya sekondari ya mfano ya WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo inatoa elimu bure kwa watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi nia ya kuanzisha shule hii yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne  325 ni kuwapatia watoto hawa elimu sawa na wenzao ambao wanawazazi.
Kazi nyingine zinazofanywa na Taasisi hiyo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwaongezea mitaji ya biashara  na kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo wanatarajia kuwafikia wanawake 60000.
Pia wanahakikisha vifo vya kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vinapungua kwa kutoa elimu kwa jamii jinsi gani inaweza kuepukana na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kutoa elimu ya jinsia na uzazi kwa vijana ili waweze kuepukana na mimba za utotoni na ugonjwa wa Ukimwi.
Akifungua mkutano huo Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia unyanyasaji wa kijinsia na utatuzi wa migogoro Zainabu Bangura alieleza kwamba katika bara la Afrika wanawake wanazalisha mali kwa asilimia 70 ya uchumi usio rasmi na asilimia 20 kwa  uchumi rasmi hivyo basi kuwanyanyasa, kuwabagua, kuwakandamiza na kuwadidimiza wanawake ni sawa na kudidimiza taifa zima.
Msemaji Mkuu katika mkutano huo kutoka Umoja wa Afrika (AU) Aisha Abdullahi ambaye ni Kamishina anayeshughulikia masuala ya siasa   alisema kuwa pamoja na ukweli kwamba ndani ya Bara la Afrika  kuna utashi mkubwa wa kisiasa na nia ya kushughulikia changamaoto za masuala ya kibinadamu, bado bara hilo linakabiliwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani na nje zaidi ya million 15.
Abdhullahi alisema, “Wakimbizi hawa wanahangaika kutafuta  mavazi, chakula na makazi maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika. Pamoja na changamoto nyingine za umaskini, uchumi duni na matatizo ya kisiasa katika baadhi ya nchi  Umoja wa Afrika umeliweka suala la wakimbizi kuwa ni moja ya  agenda zake muhimu”.
Mkutano huo ulioandaliwa na ofisi za umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu (OCHA) na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka ofisi za taasisi za kimataifa na kikanda.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...