LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi yake ya
tano kesho (Septemba 21 mwaka huu) kwa mechi huku vinara Simba wakiwakaribisha
Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi
kati ya Mgambo Shooting Stars na Rhino Rangers ya Tabora. Mtibwa Sugar itakuwa
mgeni wa Tanzania Prisons katika pambano litakalochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.
Nayo Kagera Sugar itakuwa nyumbani kwenye uwanja
wake wa Kaitaba mjini Bukoba kuvaana na Ashanti United ya Dar es Salaam katika
mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara.
Ligi hiyo itakamilisha mzunguko wa tano keshokutwa
(Septemba 22 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo Azam na Yanga zitacheza Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam huku JKT Ruvu ikikwaruzana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa
Azam Complex.
Ruvu Shooting inayokamata nafasi ya pili kwenye
msimamo wa ligi itakuwa mgeni wa Coastal Union katika mechi itakayopigwa kwenye
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
inaendelea wikiendi hii kwa mechi kumi na moja. Kundi A kesho (Septemba 21
mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Transit Camp na Green Warriors (Uwanja wa
Karume, Dar es Salaam), Tessema na African Lyon (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi).
Ndanda itacheza na Villa Squad kwenye Nangwanda
Sijaona mjini Mtwara wakati keshokutwa (Septembe 22 mwaka huu) kutakuwa na
mechi kati ya Polisi Dar es Salaam na Friends Rangers katika Uwanja wa Karume,
Dar es Salaam.
Kundi B kesho (Septemba 21 mwaka huu) ni Mkamba
Rangers dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa CCM Mkamba, na Mlale JKT itakuwa
mwenyeji wa Kurugenzi Mafinga kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Keshokutwa (Septemba 22 mwaka huu) ni Majimaji na Kimondo katika Uwanja wa
Majimaji.
Mechi za kundi C kesho (Septemba 21 mwaka huu) ni
Pamba dhidi ya Polisi Dodoma (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Stand United na
Polisi Tabora (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Kanembwa JKT itacheza na
Mwadui kwenye Uwanja wa Kawawa ulioko Ujiji. Keshokutwa (Septemba 22 mwaka huu)
Polisi Mara na Toto Africans zitacheza Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini
Musoma.
No comments:
Post a Comment