photo by www.fullshangwe.blogspot.com
Kampeni dhidi ya malaria yahamia katika pambano dhidi ya Taifa Stars na Brazil
Benjamin Sawe-Maelezo Dar Salaam
Wanafunzi 10 pamoja na walimu 13 wa Shule ya msingi Ndugumbi iliyopo magomeni katika Wilaya ya Kinondoni wamepewa nafasi ya kushuhudia mechi kati ya Taifa Stars na Brazil itakayofanyika jumatatu ijayo katika uwanja wa Taifa ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutokomeza Malaria
Nafasi hizo zilizotolewa na Rais wa TFF Leodgar Tenga zina lengo la kuhamasisha watanzania kupitia mchezo wa mpira wa miguu ikiwa ni ishara ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Bwana Tenga alisema TFF na mashirika ya African United Against Malaria na Kentaro Group wamekubaliana kushirikiana katika kupambana na ugonjwa wa Malaria kwa kutumia njia ya michezo mashuleni kwani mchezo huo umekuwa kipenzi cha watu wengi duniani.
“Bila kutokomeza ugonjwa wa Malaria inamaana hata wachezaji wa Taifa Stars wataugua ugonjwa huu hivyo kusababisha kutofanya vizuri katika michuano mingi kwa sababu ya kuugua na malaria mara kwa mara”.Alisema Bwana Tenga.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Kentoro bwana Phillipe Huber amesema kampuni yake itatoa fulana 100 na mipira kwa katiaka shule ya Ngugumbi iliyopo magomeni ikiwa na lengo la kuhamasisha wanafunzi kupitia michezo ili kupambana na malaria
Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Africa United Against Malaria Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi Christina Barrineau alisema wameanzia kutoa elimu mashuleni kwani wanafunzi watakuwa na nafasi nzuri ya kuelimisha jamii pindi wanapokuwa watu wazima.
“Unajua kampeni hii ni kampeni ya muda mrefu na tumeanzia kutoa elimu hii mashuleni kwasababu watoto ukimjenga mtoto vizuri kuhusu jambo fulani atakuwa mwalimu mzuri wa kuelimisha jamii juu ya athari za ugonjwa wa malaria”.Alisema Bi Barrineau
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Ndugumbi Warda Kibuga alisema wanashukuru TFF pamoja na mashirika ya Africa United Against Malaria na Kentaro Group kwa kuwapatia vifaa mbalimbali vya michezo.
“Tunashukuru kwa vifaa mlivyotupatia na tunawahakikishia tutavitumia vifaa hivi vya mpira wa miguu hasa kipindi cha mapumziko wakati wa mazoezi na mechi kwa kutoa elimu ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa malaria kwa wapinzani wetu na hata sisi wenyewe”.Alisema.
Pia alisema hiyo watakayopata kipindi cha mpira kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali wa malaria wataisambaza katika jamii ili ipate elimu juu ya kujikinga na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment