Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa (kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu na kiongozi wa
Taasisi ya Tanga Women Development Initiative (TAWODE) wakizundua mradi
huo.
Watoto wakike ambao ndio walengwa wa mradi huo wakiwa na vyeti vyao.
Watoto wa Kike wakifuatilia uzinduzi wa taasisi yao.
Moja ya vipeperushi
OKTOBA
11 ya kila mwaka ni siku ya mtoto wa kike duniani. Mkoani Tanga
waliadhimisha siku hiyo ya mtoto wa kike kwa kuzindua mradi maalum wa
kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga chini ya Taasisi ya Tanga
Women Development Initiative (TAWODE).
Mgeni
rasmi katika uzinduzo huo uliofanyika uwanja wa michezo wa Mkwakwani
alikuwa Mhe Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, na kuhudhuriwa pia na
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu na Wakuu wa Wilaya za
Mkoa wa Tanga wakiongozwa na Halima Dendegu .
Akizungumzia
uzinduzi huo Naibu Waziri mwenye dhamana hiyo ya Jinsia, Ummy Mwalimu
alisema kuwa amefurahishwa sana na uzinduzi wa mradi huo.
“Kupitia
mradi huu ninafurahi kuona nikitekeleza kwa vitendo dhamira yangu kama
kiongozi - 'niliechaguliwa' na wanawake wa mkoa wa Tanga- kuchangia
kuboresha maisha ya Wanawake na Watoto wa Mkoa wa Tanga”, alisema
Mwalimu.
Pia shukrani zilienda kwa Balozi wa Denmark nchini, Johnny Flento kwa kuunga mkono jitihada hizo.
Mradi
huo utatekelezwa ktk Wilaya za Pangani, Muheza, Mkinga, Lushoto na
Tanga Mjini, umelenga kuchochea uwezo na ubora wa wasichana (wa umri wa
miaka 10-24), kutambua weledi na umuhimu wao kwa maendeleo yao na ya
jamii zao.
Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa alisema kuwa kupitia mradi huo Mkoa
umedhamiria kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wasichana waliopo katika
shule za Serikali za Msingi na Sekondari, kuboresha hali ya afya ya
uzazi, kupunguza mimba za mapema, ndoa za utotoni na maambukizi ya VVU.
“Tumepanga
kuwafikia moja kwa moja wasichana 16,000 na zaidi ya 100,000 kupitia
njia mbalimbali ikiwemo mabango, Radio jingles (Mwambao FM 106.0),
matamasha ya wasichana na njia nyingine mbalimbali,”alisema Galawa.
Aidha
Wasichana 1,000 waliopo shuleni na wanaoishi ktk mazingira magumu
wataingizwa katika Mfuko wa Bima ya afya ili kuweza kupata huduma za
afya bure.
Endapo
jitihada hizo zitazaa matunda zitachochea maendeleo ya wanaTanga ambao
wamekuwa na utayari wa kupokea ushauri na mawazo ya wadau mbalimbali
juu ya Utekelezaji mzuri wa Mradi huo.
No comments:
Post a Comment