Na Mashaka Mhando, Handeni.
MBUNGE wa Handeni Dkt Abdallah Kigoda, ameaahidi kushirikiana na
kuwasaidia waandaaji wa Tamasha la Utamaduni na Michezo lililopewa jina la
‘Handeni Kwetu’ litakalofanyika Desemba 14 mwaka huu mjini Handeni, mkoani
Tanga, ili kuunga mkono jitihada za wadau katika suala zima la utamaduni na
maendeleo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Abdallah Kigoda, ambaye pia ni Mbunge wa Handeni.
Akizungumza wakati akizindua kisima cha maji katika
soko la zamani lililopo katika mji wa Chanika, Dkt Kigoda, alisema anaunga mkono
tamasha hilo ambalo litaibua fikra na mtizamo mpya wa utamaduni miongoni mwa
wananchi wilayani hapa.
“Waandaji wa Tamasha la Utamaduni wamenipa taarifa
za kufanyika tamasha hilo nami kama mbunge wa jimbo hili sina budi kuwaunga
mkono kufanikisha tamasha hilo na nitashirikiana nao,” alisema Dkt Kigoda
ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Dkt Kigoda alisema suala la utamaduni ni suala
mtambuka ambalo linagusa mioyo ya wananchi wengi hivyo unapoweka tamasha kwa
ajili ya utamaduni wa ngomalicha ya kuwapa burudani wananchi hutoa hamasa kwa
vijana kupenda mila na utamaduni hasa suala na ngoma za asili.
Mbunge huyo alitoa wito kwa wananchi wilayani humo
na wale waliopo nje ya handeni kujitokeza kushiriki tamasha hilo ili kuibua
mawazo mapya juu ya masuala ya utamaduni na michezo yaliyokosa msisiko kutokana
na kutopewa kipaumbele.
Mbunge huyo, aliahidi kusaidia tamasha hilo baada ya
kupewa taarifa na mwandaaji wake Kambi Mbwana.
Wadhamini waliothibitisha kushiriki katika
tamasha hilo ni pamoja na Phed Trans inayomilikiwa na Yusuphed Mhandeni, Grace
Products, Screen Masters, Dullah Tiles $ Construction Ltd, Katomu Solar
Specialist na Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.
Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware,
SmartMind & Partners chini ya ANESA COMPANY LIMITED, ikidhamini kwa kupitia
kitabu cha ‘NI WAKATI WAKO WA KUNG'AA, Screen Masters, Saluti5.com, Lukaza
Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu Blog.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alisema kuwa
wataalamu wanafanya utafiti kwa ajili ya kuchimba kisima katika uwanja wa mpira
wa Azimio ambao unakarabatiwa ili uweze kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu na
klabu ya Mgambo JKT.
Alisema tayari ametoa kiasi cha shilingi milioni 250
kutoka katika mfuko wake wa maendeleo ya jimbo ili kuukarabati uwanja huo ambao
tayari umeoteshwa nyasi mpya na kujengwa vyumba vya kubadilishia ngu wachezaji
pamoja na jukwaa kuu.
No comments:
Post a Comment