Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, April 30, 2012

TRA YAPUNGUZA KODI YA BODABODA


Venance George, Morogoro
MAMLAKA ya Mapato (TRA) mkoani Morogoro, imewapunguzia kodi wafanyabishara ya pikipiki maarufu kama bodaboda kutoka Sh95,000 hadi Sh35,000 kwa mwaka kwa pikipiki moja.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na kaimu Meneja wa mamlaka hiyo mkoani hapa, Kilomba Kanse na kuthibitishwa na Meneja wa Mkoa, Hakim Kimungu, hatua hiyo imefikiwa na mamlaka kufutia ombi la wafanyabishara hao kutaka kupunguziwa kodi hiyo.

Kimungu alisema kuwa wafanyabishara hao kupitia chama cha waendesha pikipiki mkoani Morogoro (CCWPM) waliwasilisha maombi kwenye mamlaka hiyo wakitaka kupunguziwa kodi na kutoa sababu kuwa idadi ya pikipiki mkoani Morogoro imeongezeka huku idadi ya wateja ikiendelea kuwa ile ile, hali ambayo imedaiwa kupunguza mapato yao.

“Sisi sababu hiyo tuliiona kuwa ni ya msingi, kwa vile mkoa wa Morogoro kwa sasa unapikipiki nyingi kuliko pengine mikoa yote ukiachilia mkoa wa Dar es Salaam, ongezeko hilo limesababisha idadi ya wateja kupungua na kupungua kwa mapato yao,” alisema Meneja huyo.

Aliongeza kuwa TRA mkoa wa Morogoro imekuwa na mazungumzo na mwenyekiti wa CCWPM, Anamwikira Massawe, na kufikia makubaliano hayo na kwamba hatua hiyo ilizingatia vigezo vya mamlaka hiyo ambapo walipakodi kama wafanyabiashara ya bodaboda miaka mitatu iliyopita walikadiriwa kulipa kodi ya Sh95,000 kutokana na kipato chao kufikia kati ya Sh3 milioni na Sh7 milioni kwa mwaka.

Alisema kutokana na ongezeko la pikipiki mapato ya wafanyabishara hiyo yameonekana kushuka mpaka kufikia chini ya Sh3 milioni kwa mwaka kiwango ambacho kinaipa mamlaka uwezo kuwatoza Sh35,000 kwa mwaka, kiwango ambacho ni cha chini kwa walipakodi wa kukadiriwa wasiofanya mahesabu.

Kimungu alisema kuwa punguzo hilo la kodi litakuwa ni kwa wafanyabishara wa bodaboda wote mkoani Morogoro, lakini alisisitiza kwamba wenye pikipiki nyingi zaidi ya moja watatozwa kulingana na makadirio ya faida ya mapato yao kwa mwaka.

“Pamoja na punguzo hilo la kodi TRA tutaendelea kufanya uchunguzi wetu kwa njia mbalimbali na pale ambapo tutajiridhisha kuwa mapato ya waendesha pikipiki hao yameongezeka tena tutarudi kuwatoza kiasi kile kile cha Sh95,000 kwa mwaka na wale wenye pikipiki nyingi tumeanza kuwalazimisha kufanya mahesabu ili watozwe kodi kulingana na hesabu hizo,” alisema.

Hata hivyo kwa mujibu wa barua ya mamlaka hiyo ya kujibu ombi la bodaboda imeeleza kuwa bodaboda ambao wamekwisha kadriwa kwa kulipa Sh95,000 kwa mwaka huu watalipa punguzo la kodi hiyo mwakani lakini ambao hawajakadiriwa na hawajalipa kodi hiyo watalipa kodi mpya ya Sh35,000 kodi ambayo itaanza kutozwa April 27, 2012.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa CCWPM, aliipongeza mamlaka hiyo kwa hatua ya kuwapunguzia kodi na kuongeza kuwa uamuzi huo utawafanya bodaboda kwenda kulipa kodi kwa hiari badala ilivyokuwa mwanzo ambapo wengine walikuwa wakilipa kodi kwa kusukumwa.

Massawe amewataka waendesha pikipiki mkoa wa Morogoro kushirikiana na mamlaka ya mapato ili kodi mpya iliyopendekezwa iweze kukusanywa kwa urahisi na kwamba hatua hiyo pia itaiwezesha mamlaka kukuzanya mapato zaidi kwa kuwa walipa kodi hiyo wataweza kuongezeka. Chanzo; Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...