Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, November 7, 2013

Yanga yarejea kileleni, Azam, Mbeya City zawekwa rekodi zikitoka sare ya 3-3,Mwagane Yeya apiga hat trick


Azam wakishangilia moja ya mabao yao msimu huu
Mbeya City wakiomba dua kuwasaidia wafanye vyema katika mechi zao
MSHAMBULIAJI Mwagane Yeya ameingia kwenye rekodi ya wafungaji wa hat trick msimu huu baada ya jioni ya leo kutupia mabao matatu wavuni wakati timu yake ya Mbeya City ikilazimisha sare ya mabao 3-3 na Azam.
Mchezaji huyo anakuwa wa tatu kufunga mabao matatu katika mechi moja na mzawa wa pili baada ya Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar kuvunja rekodi iliyokuwa imedumu kwa misimu miwili tangu iwekwe na Juma Semsue wa Polisi Dodoma mwaka 2010-2011.
Yeya alifunga mabao hayo katika pambano la funga nikufunge baina ya timu yake na Azam lililochezwa kwenye uwanja wa Chamazi na kuzifanya timu hizo kugawa pointi na kuipisha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mabao yake aliyafunga katika dakika ya 30, 50 na 73 na kuwafanya washambuliaji wa Azam kuwa na kazi ya kuyarejesha ambapo John Bocco 'Adebayor' alifunga bao la kusawazisha la pili kabla ya Mcha Khamis Vialli kuchomoa bao la tatu dakika ya 83 na kuzifanya timu hizo zigawane pointi na kuweka rekodi ya kutofungika duru zima la kwanza.
Timu hizo ndizo pekee hazijafungwa katika ligi mpaka sasa na zikiwa zimemaliza mechi zake zikiwa na ponti 27 kila mmoja wakizidiwa na Yanga waliorejea kileleni wakiwa na pointi 28 baada ya kuinyuka Oljoro JKT mabao 3-0 kwenye uwanja wa Taifa.
Bao la tatu la Azam lilifungwa na Humphrey Mieno aliyetangulia kufunga dakika ya 13 tu ya mchezo kwa kichwa kabla ya Yeya kusawazisha na kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa ya bao 1-1.
Katika uwanja wa Taifa Yanga ilipata mabao yake kupitia Simon Msuva aliyefunga katika dk ya 23 kabla ya Mrisho Ngassa kufunga bao la pili dakika ya 30 na Jerry tegete kuongeza bao jingine dakika ya 54 na kuhitimisha ushindi wa mechi nne mfululizo wote ukiwa kwa timu za maafande na kurejea kileleni hadi mwakani.
Katika mechi nyingine ya mjini Tabora matokeo ni kwamba timu ya Rhino Rangers ikiwa nyumbani imeshindwa kufurukuta kwa kulazimishwa suluhu na Prisons ya Mbeya.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...