Na mwandishi wetu, Dodoma
Naibu Kamishna wa Polisi na Kamanda
wa Kikosi cha Polisi Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
amekubaliana na haja ya kuanzisha mafunzo katika vyombo vya habari vya
kijamii kama facebook ili kutanua uwanja zaidi wa elimu ya usalama
barabarani hasa kwa vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa ajali.
Aidha amesema Polisi wanafikiriia
kuanzisha mfuko wa kielektroniki wa ulipaji wa faini kwa makosa ya
barabarani ili kuongeza kasi ya udhibiti na kuondoa tuhuma za rushwa.
Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa wiki
wakati akizungumza na wanahabari na watendaji kutoka redio za jamii
nchini mjini Dodoma, katika warsha ya siku nne ya wadau wa utekelezaji
wa mradi wa uchaguzi unaolenga kuboresha Demokrasia na Amani nchini
(DEP) kuelekea uchaguzi mkuu ujao iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kufadhiliwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo (UNDP).
washa ya siku nne ya wadau wa
utekelezaji wa mradi wa uchaguzi unaolenga kuboresha demokrasia na amani
nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Unesco , Bw. Al Amin Yusuph, akisalimiana na Naibu Kamishna wa Polisi
na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mohamed
Mpinga, mara baada ya kuwasili kwenye warsha hiyo iliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.
Kauli yake hiyo ilifuatia hoja
iliyotolewa na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika
la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), Bw. Al Amin
Yusuph, ambaye aligusia redio za jamii katika kusambaza habari zenye
kulenga kuokoa maisha na mali kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Mpinga ambaye pia ni kamanda wa
kikosi cha usalama barabarani alisema katika mada yake kwamba changamoto
kubwa ni kutekeleza sera ya kuhakikisha kwamba hakuna kifo wala
majeruhi katika ajali za usalama barabarani.
Akielezea hali halisi ya ajali
barabarani huku akikariri takwimu za Benki ya Dunia na Shirika la Afya
Duniani (WHO) kamanda Mpinga alisema kwamba utafiti unaonesha katika
kila wakazi 100,000 duniani 24 hufa katika ajali za barabarani ambapo
vijana na watu maskini ndio wapo katika hatari kubwa zaidi.
Aidha alisema takwimu zaidi kutoka
WHO zinasema kwamba watu million 1 na laki tatu hufa kila mwaka duniani
hapa kwa ajali huku ikibainisha kwamba asilimia 75 ya watu wanaojeruhiwa
na kufa wanatoka katika nchi maskini ambazo hazina magari mengi kama
zile zilizoendelea.
Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Unesco , Bw. Al Amin Yusuph
(kushoto) akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Naibu
Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Usalama Barabarani
nchini ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, kutoa mada kwa watendaji wa redio za jamii
nchini. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa mtandao wa redio za jamii nchini
(COMNETA) ambaye pia ni Meneja wa redio jamii Sengerema FM ya mkoani
Mwanza Bw. Felician Ncheye.
Alisema pamoja na takwimu hizo za
kutisha za duniani, nchini kwetu pekee watu 4000 hufa kila mwaka
kutokana na ajali na mwaka uliopita walikufa watu 4002.
Akitoa mada katika mafunzo hayo
alisema kwamba ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na binadamu
ambapo asilimia 75 za ajali zote husababishwa na makosa ya kibinadamu.
Alisema utafiti unaonesha kwamba
makosa hayo chanzo chake ni uzembe, ulevi, mwendo kasi, kutozingatia
sheria, uchovu wa madereva na matumizi ya vyombo vya moto.
Aidha uzembe wa waendesha pikipiki ndio unabeba asilimia 20 hadi 30 ya ajali zote.
Alisema kufunguliwa kwa biashara ya
pikipiki kubeba abiria kumewaingiza vijana wengi ambao wengi wao si
wataalamu wakikosa sifa ya kuendesha vyombo hivyo vya moto huku wakiwa
vinara wa kuvunja sheria barabarani kwa vitendo.
Naibu
Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Usalama Barabarani
nchini ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, akiwasilisha mada
kwa watendaji wa redio jamii nchini (hawapo pichani) waliokuwa
wakihudhuria warsha ya siku nne ya wadau wa utekelezaji wa mradi wa
uchaguzi unaolenga kuboresha Demokrasia na Amani nchini (DEP) kuelekea
uchaguzi mkuu ujao iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo (UNDP) iliyoamlizika mwishoni mwa
wiki mjini Dodoma. Kushoto ni Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na
Tehama wa Unesco , Bw. Al Amin Yusuph na Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa
mtandao wa redio za jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni Meneja wa redio
jamii Sengerema FM ya mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye.
Madereva hao alisema wanaendesha kasi, hawavai kofia ngumu na kubeba abiria kwa mtindo wa mishikaki.
Akifafanua zaidi amesema kwamba
pamoja na madereva wa pikipiki kuongoza kwa kuvunja sheria hali za
barabara kama kukosekana kwa alama, muundo wa barabara zenyewe, utelezi ,
uchakavu wa vyombo na hali ya hewa vimekuwa visababishi vya ajali.
Kamanda alitaka vyombo vya habari
vya redio za jamii kuelimisha madereva matumizi sahihi ya barabara kwa
kuwaita wataalamu kuelezea mambo hayo bila chumvi wala kuharibu nidhamu
na maisha .
Alisema mathalani maeneo ya mnadani
madereva wamekuwa wakivunja sheria hasa upakiaji wa mizigo
isiyozingatia usalama wa abiria waliomo.
Alisema jeshi la polisi limechukua
mikakati kadhaa kuwezesha kukabiliana na hali ya usalama barabarani hasa
kwa kuanzisha ukamataji wa makosa hatarishi katika usalama wa barabara.
Makosa hayo ni mwendokasi, ulevi,
uendeshaji wa hatari na uzidishaji wa abiria alisema faini zinazotolewa
zimefanya kupungua kwa ajali kutoka elfu 17 hadi elfu 11.
Alisema mikakati mingine ni utoaji
wa elimu kwa kupitia vyombo vya habari na kushukuru kwamba elimu hiyo
anaona inasaidia. Alisema wanatoa elimu kupitia televisheni , redio na
vyombo vya habari vya kijamii.
Pia aliutaja mkakati mwingine ni
kuboresha mifumo ya utendaji kwa kuainisha maeneo yanayotokea ajali mara
kwa mara, ukusanyaji wa takwimu na kubadili mfumo wa ukaguzi barabarani
kwa kuanzisha maeneo maalumu ya kukagulia magari kwa undani.
Pia kunatengenezwa mfumo wa nukta ambapo dereva anapofanya makosa pointi zinaondolewa na zikimalizika anapokonywa leseni.
Kuhusu ulipaji wa faini kupitia
benki na njia nyingine za elektroniki alisema zitarahisha utendaji wa
polisi na kuondoa tuhuma za rushwa na pia kuwafanya watu kuwa waangalifu
zaidi.
Aidha amesema wanatengeneza
utaratibu kwa kushirikiana na wadau wengi kutengenezwa kanuni ya ulazima
wa madereva kurejea shule kwa mafunzo hasa kutokana na kubadilika mara
kwa mara kwa miundombinu ya barabara na teknolojia ya magari.
Sehemu
ya wadau/watendaji wa redio jamii wa utekelezaji wa mradi wa uchaguzi
unaolenga kuboresha Demokrasia na Amani nchini (DEP) kuelekea uchaguzi
mkuu ujao wakifuatilia kwa umakini mada iliyowasilishwa na Kamanda
Mpinga kwenye warsha hiyo.
Hata hivyo alisema pamoja na
mikakati hiyo na mingine Jeshi la Polisi linakabiliwa na changamoto
zinazoambatana na bajeti ndogo ya kuiwezesha kununulia vifaa vya kazi
kama speed radar za kisasa na mifumo muafaka ya kusimamia usalama
barabarani ambapo kwa sasa kila tatizo wanasukumiziwa polisi iwe ni taa
mbovu za barabarani au mashimo.
Changamoto nyingine ni wananchi wenyewe kukosa utamaduni wa kuheshimu sheria mpaka waone polisi.
Alivitaka vyombo vya redio jamii
kufundisha wananchi na wala sio kuchochea wao wazidi kuvunja sheria na
kuitoa mfano wa matuta barabarani ambayo yanadaiwa na wananchi na kusema
hiyo si dawa bali elimu kwa wananchi kuhusu usalama barabarani na namna
ya kudhibiti ajali.
Naye Afisa Miradi ya Mawasiliano,
Habari na Tehama wa Unesco , Bw. Al Amin Yusuph akimkaribisha Kamanda
Mpinga azungumze alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili redio za
jamii kujiuza kw apamoja katika kuhudumia umma na kujiendeleza.
Alisema redio ndio njia pekee ya
kuwafikia watanzania wengi hasa kwa kuzingatia kwamba watumiaji wa
vyombo vingine ni wachache hasa kutokana na kukosekana kwa nishati na
pia kuwa mbali na maeneo yanayotangaza habari.
Wasaidizi
wa Kamanda Mpinga wakigawa machapisho mbalimbali yanayotoa elimu ya
usalama barabarani kwa washiriki wa warsha hiyo iliyomalizika mwishoni
mwa juma mjini Dodoma.
Reportuer
wa warsha ya wadau wanaotekeleza mradi wa uchaguzi iliyomalizikia
mwishoni mwa juma mjini Dodoma Mchungaji Privatus Karugendo akihoji
suala la baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto wanaotumia simu za
viganjani pindi wawapo barabarani kitu ambacho ni hatari kwa usalama
wao.
Baadhi ya machapisho yaliyogawiwa kwa watendaji wa redio jamii nchini yanayotoa elimu ya usalama barabarani.
Baadhi
ya washiriki wa warsha hiyo wakipitia machapisho hayo yaliyotolewa na
Kitengo cha Polisi Usalama Barabarani kwenye warsha hiyo.
No comments:
Post a Comment