Michuano
ya Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu iliyokuwa ianze kutimua vumbi
Novemba 22 mwaka huu kwa mechi kumi katika viwanja vitano tofauti
imesogezwa mbele hadi Desemba 6 mwaka huu.
Mechi
hizo zimesogezwa ili kutoa fursa ya kukamilisha maandalizi mbalimbali
ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania
Bara.
Mikoa
yenye timu katika ligi hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa,
Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani,
Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.
MASHINDANO YA TAIFA YA U12 YASOGEZWA
Mashindano
ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12 yanayoshirikisha
kombaini za mikoa yote ya Tanzania yatafanyika jijini Mwanza kuanzia
Desemba 30 mwaka huu hadi Januari 5 mwakani.
Awali
mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba 6 mwaka huu, lakini
yamelazimika kuyasogeza ili kutoa fursa ya kukamilika kwa matengenezo ya
viwanja vitatu ambayo vitatumika.
Kila
timu ya mkoa inatakiwa kuwa na ujumbe wa watu 16, wakiwemo wachezaji 14
na makocha wawili katika mashindano hayo ya timu yenye wachezaji saba
(7 aside).
Timu
zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza kuanzia Desemba 28 mwaka huu tayari
kwa ajili ya uhakiki wa umri na taratibu nyingine za mashindano. Timu
zote zitafikia katika shule ya Alliance (Alliance Schools).
Wachezaji
wanaotakiwa kushiriki mashindano hayo ni wenye umri chini ya miaka 12,
hivyo ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 2003 na kuendelea.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MUNYUKU, KARASHANI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya
waandishi wa habari Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea
jana (Novemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba
huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari
nchini kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa
mpira wa miguu nchini kupitia kalamu zao.
Munyuku
alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati
Karashani kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya
habari ikiwemo kampuni ya New Habari 1996 akiripoti habari za mpira wa
miguu.
Tunatoa
pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA), na kampuni ya New Habari 1996 na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment