Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, February 19, 2014

CCM yawapa onyo kali Makada wake wanaodaiwa kuunyatia Urais kabla ya kipyenga kupulizwa


Kati ya tarehe 13/02/2014  na tarehe 18/02/2014 kumekuwa na mfululizo wa vikao kadhaa vya Chama kitaifa vilivyoshughulikia suala la maadili ndani ya Chama.

Vikao hivyo ni pamoja na Kamati Ndogo ya Udhibiti tarehe 13-14/02/2014, Tume ya Udhibiti na Nidhamu 18/02/2014 na Kamati Kuu tarehe 18/02/2013.

Waliohojiwa katika mfululizo wa vikao hivi ni wafuatao:-

1.            Ndg. Frederick Sumaye
2.            Ndugu Edward Lowasa
3.            Ndugu Bernard Membe
4.            Ndugu Stephen Wassira
5.            Ndugu January Makamba
6.            Ndugu William Ngeleja

Baada ya kuwahoji ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza adhabu.  Mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.

Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo:-

1.        Walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

2.       Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.  Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.
 
Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi.

Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:-

“Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.”

Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za Chama.

Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.

Imetolewa na:-

Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI,
18/02/2014

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...