Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, May 24, 2012

WAZIRI MAKALA AIKABIDHI BENDERA TWIGA STARS


Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Twiga Stars) inayotarajia kuondoka leo saa 11.05 jioni kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwenda Ethiopia imekabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.

Twiga Stars yenye msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu Equatorial Guinea.

Mechi hiyo itafanyika Mei 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Addis Ababa wakati ile ya marudiano itachezwa Juni 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.

Wachezaji walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.

Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano (Daktari wa Timu).

Twiga Stars ambayo msafara wake unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu saa 6 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...