Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza
na Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Dkt. Yassir Mohammed Ali, wakati alipofika
Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo Juni 05, 2012 kwa mazungumzo.
Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Jumanne ya
Tarehe 05 Juni 2012 amekutana na Mabalozi wa nchi za Sudan na Msumbiji
waliomtembelea ofisini kake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi wa kwanza kufika
alikuwa Balozi wa Sudan nchini Tanzania Mheshimiwa Dkt. Yassir Mohamed Ali
ambaye amekutana na Makamu wa Rais kwa mara ya kwanza na katika kujitambulisha
kwake akaelezea nafasi ya Tanzania katika kuhakikisha Bara la Afrika linabakia
kuwa na amani na utulivu.
Balozi Mohammed
alimwambia Makamu wa Rais kuwa wafanyabiashara kutoka Sudan wamekuwa
wakishiriki katika uwekezaji nchini na bado wapo ambao wana nia ya kufanya
hivyo na kwa kuanzia wafanyabiashara hao watashiriki katika maonyesho ya
Biashara ya Kimataifa maarufu kama Saba Saba yatakayofanyika mwaka huu. Balozi
huyo alieleza pia kuwa, Sudan inadumisha uhusiano wake na Tanzania katika
kuhakikisha nchi mbili zinabakia kuwa na lengo moja kubwa la kuwapatia wananchi
maendeleo.
Kwa upande wake
Mheshimiwa Makamu wa Rais, yeye alimkaribisha Balozi Mohammed na kumwahidi kuwa
Tanzania itazidi kutumia nafasi yake katika kuhamasisha amani hasa sasa ambapo
nchi ya Sudan iko katika mgogoro na Sudan ya Kusini.
Balozi Amour Zacarias
Kupela wa Msumbiji, yeye sambamba na kumuaga Mheshimiwa Makamu wa Rais
alimwambia kuwa amefurahi sana kuwepo nchini Tanzania na kwamba anaithamini
nchi hii kama nyumbani kutokana na uwezo wake wa kudumisha amani na pia kwa
nafasi yake katika kuhakikisha wananchi wa Msumbiji wanakuwa huru na wanaishi
kwa amani kama ilivyo sasa.
Balozi huyo alisema
serikali ya Msumbiji inatumia fursa zake za kuhakikisha inakuza kilimo ili
kutoa nafasi ya kuwepo chakula cha kutosha nchini humo na
pia akafafanua kuwa
hali ya kisiasa nchini mwake kwa sasa ni shwari na hivyo wananchi wa ajukumu
moja tu la kujitafutia maendeleo.
Balozi Maricias
alifafanua kuwa upo umuhimu wa kukuza nafasi za kubadilishana wanafunzi kati ya
Msumbiji na Tanzania kwani kama haitafanyika hivyo ni rahisi wananchi wa nchi
hizi kusahau historia ya namna nchi hizi mbili zilivyoshirikiana katika kipindi
cha kupigania uhuru.
Makamu wa Rais
alimueleza Balozi Maricias kuwa, Tanzania inashukuru sana kwa mchango wake
alioutoa kama Balozi na pia katika kazi alizofanya kabla ya kuwa Balozi.
Alimtakia kila la kheri katika kazi zake mpya huku akimhakikishia kuwa Tanzania
itabakia na mahusiano chanya na Msumbiji katika kipindi chote.
No comments:
Post a Comment