Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, May 4, 2012

KAMPUNI YA BIA TANZANIA (TBL) KUPITIA BIA YA SAFARI KUDHAMINI MASHINDANO YA POOL TABLE KWA VYUO VYA ELIMU YA JUU


Baadhi ya Wachezaji wa Pool kutoa Vyuo Mbali mbali wakicheza mchezo huo ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa Mashindano hayo.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager leo imetangaza rasmi kudhamini kwa mara nyingine tena mashindano ya mchezo wa Pool Table kwa vyuo vya elimu ya juu hapa Tanzania. Mashindano haya yajulikanayo kama “Safari Lager Higher Learning Pool Championships” yanafanyika kwa mwaka wa tatu sasa, Safari Lager imekuwa wadhamini wakuu wa mashindano haya kwa miaka yote hii mitatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo meneja wa Safari Lager,Oscar Shelukindo alisema nia hasa ya kudhamini mashindano haya ni kuwapa wanafunzi burudani baada ya ratiba ngumu za masomo ili waweze kupumzisha akili warudi wakiwa na ari mpya. Mapumziko husaidia akili kufanya kazi kwa haraka na kuwa na ubunifu zaidi.

Shelukindo aliendelea kusema “Mbali na kupumzisha akili, michezo husaidia kuwakutanisha watu mbalimbali, kujenga afya bora na katika mazingira yetu ya sasa mchezo wa Pool umekua zaidi na unaweza kuwa kama fani nyingine zinazomuingizia mchezaji pesa”. Safari Lager imekuwa wadhamini wa mchezo wa Pool toka mwaka 2008, imedhamini mashindano ya ndani na ya nje ya nchi pia. Imedhamini timu ya Taifa ya mchezo wa Pool kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo wa Pool nchini Ufaransa mwezi wa kumi mwaka 2010 ambapo timu yetu ilifanya vizuri.

Naye katibu wa chama cha mchezo wa Pool Tanzania (TAPA),Amos Kafwinga alisema mashindano haya yanaanzia kwa vyuo kushindana katika ngazi ya mkoa na baadae mikoa yote itashindana katika ngazi ya taifa ili kupata mshindi wa jumla kwa vyuo vyote.

Mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi kutimua vumbi katika mkoa wa Morogoro Jumamosi ijayo tarehe 12 May 2012. Mashindano ya mwaka huu yatahusisha wanafunzi wa vyuo vilivyo katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Dar Es Salaam. Mashindano ya taifa mwaka huu yatafanyika katika mkoa wa Iringa mwanzoni mwa mwezi wa sita.

Mwaka jana chuo cha Usimamizi Wa Fedha (IFM) kiliibuka na ushindi katika mashindano ya kitaifa yaliyofanyika mkoani Dodoma, walijipatia kikombe na jumla ya shilingi milioni mbili na laki tano. Akizungumzia ushindi huo,Charles Venance ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho na kiongozi wa timu ya pool ya chuo alisema fedha hizo ziliwasaidia katika mahitaji mbalimbali ya masomo. Alisema “Tumejiandaa vizuri sana mwaka huu na kwa hakika ushindi utabaki IFM, vyuo vyote vitakubali kwamba IFM ni moto wa kuotea mbali kwenye Pool!”.

Akitoa shukrani kwa Safari Lager kwa niaba ya Chama cha Mchezo wa Pool Tanzania (TAPA), Mwenyekiti wa chama hicho,Isaac Togocho alisema “Taswira ya mchezo wa pool hapa nchini imebadilika kwa kiasi kikubwa na sasa inawavutia vijana wa kaliba mbalimbali kwani si mchezo wa kupotezea muda tena kama wengi walivyodhania, Pool ni miongoni mwa michezo inayokua kwa kasi kubwa na kuwapatia kipato wachezaji na vijana kwa ujumla. Hii yote imetokana na Bia ya Safari Lager kukubali kuudhamini mchezo wa Pool table. Kwa niaba ya chama tunatoa shukrani nyingi sana na kuomba Safari Lager iwe nasi ili tuendelee mbele zaidi”.

Shelukindo alizitaja zawadi za washindi katika ngazi ya mikoa kuwa timu itakayoshinda itajipatia kitita cha shilingi laki tano, washindi wengine watajipatia shilingi laki tatu kwa mshindi wa pili, laki mbili na laki moja kwa mshindi wa nne. Washindi kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wa kiume watajipatia shilingi laki moja na nusu kwa bingwa na laki moja kwa mshindi wa pili.

Wachezaji wa kike watajipatia laki moja kwa bingwa na shilingi elfu hamsini kwa mshindi wa pili. Mshindi katika ngazi ya taifa ataibuka na kikombe pamoja na jumla ya shilingi milioni mbili na nusu taslim (2,500,000), jumla ya shilingi milioni tisa na laki tano zitatolewa kama zawadi katika michuano ya ngazi ya taifa.

Shelukindo alimalizia kwa kutoa shukrani kwa wanywaji wa bia ya Safari Lager na wachezaji wote wa mchezo wa Pool kwa ujumla, aliwaomba wajinoe kwani Safari Lager inadhamini tena mashindano ya kitaifa ya mchezo wa pool ambayo yataanza hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...