MBUNGE
wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya Dr.Mary
Mwanjelwa amekanusha uvumi ulioripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari
hapa nchini kuwa anatarajia kukihama chama hicho na kujiunga na Chama
cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Alisema
taarifa hizo ni uzushi na uongo kwa sababu yeye ni kada wa CCM wa siku
nyingi ambaye amepewa dhamana na chama hicho kugombea ubunge kupitia
jumuiya ya wanawake hivyo hatarajii kuwageuka kwa sababu bado anayo
dhamana ya kuendelea kuwa Mbunge.
Alisema,
taarifa hizo zimenishtua sana, na hata wapiga kura wangu nao wamepata
mshtuko mkubwa na wakanipigia simu ili kutaka kupata ukweli kutoka
kwangu hivyo nimeona ni vizuri nitoe ufafanuzi.
Alisema
yeye ni mbunge wa wananchi wote mkoani hapa, hana matatizo yeyote na
chama hivyo haielewi sababu za kumfanya ahame chama chake na kujiunga na
CHADEMA, kwa sababu ya uteuzi wa baraza jipya la mawaziri.
"Mimi
ni mbunge kwa tiketi ya CCM na pia ni kada wa chama ambacho ndicho
kilichonipitisha kugombea nafasi ya ubunge viti maalumu, na hatimaye
nikafanikiwa kuchaguliwa sasa iwaje leo nikihame chama,"alihoji Mbunge
huyo.
Aliongeza
habari zilizoripotiwa ni za uongo, na kuwa kamwe hawezi kuingilia
uteuzi wa Rais Kikwete katika kuwateua mawaziri, kwani hayo ni mambo
ambayo hayamhusu kabisa.
Dk.Mary
alisema yeye amekwenda Bungeni kuwawakilisha wananchi wa mkoa wa Mbeya,
sikwenda Bungeni kwa sababu ya kutaka kuwa Waziri, hizo ni nafasi za
uteuzi na mwenye mamlaka hiyo ni Rais Kikwete.
Mbunge
huyo wa viti maalum Mbeya, aliongeza hivyo ni vyema waandishi wa habari
waache kuandika habari za kuchafuana, kuharibiana bali wafuate misingi
na maadiri yanayolinda tasnia ya habari.
Alisema
iwapo mwandishi anakuwa amepata taarifa ni vyema amfuate muhusika ili
kupata ukweli juu ya habari anayotaka kuiandika iwapo ina ukweli wowote
ndani yake.
Aliongeza
kama hayo yalikuwa ni maoni ya wananchi, anashindwa kuelewa yeye
anaingizwaje katika habari hiyo, kwani ana mkataba wa kuwatumikia
wananchi kwa miaka mitano na amebakiza miaka mitatu.
"Siwezi
kuhamia CHADEMA, kwani CCM haijanifanyia kosa lolote, sikwenda Bungeni
ili niteuliwe kuwa Waziri, kikubwa kwangu ni kuingia Bungeni kwa ajili
ya kuwawakilisha wananchi wangu wa mkoa wa Mbeya" alisema Dk.Mary.
Kwa
mujibu wa Mwanjelwa alisema kuwa ni kweli alizungumza na Mwandishi
aliyeandika habari hizo na kwamba mwandishi huyo alikuwa akitaka kupata
ufafanuzi wa uvumi ulioenea ya kwamba kuna baadhi ya wananchi wanataka
kwenda kumuona ili wamshawishi akihame chama kwa sababu ya Rais
hakumteua kwenye Baraza jipya la Mawaziri.
"Mimi
nilimjibu mwandishi huyo ya kwamba huo ni mtazamo wa wananchi lakini si
wa kwangu "alisema Mwanjelwa huku akisisitiza kuwa hicho ni kipindi
chake cha kwanza kuingia Bungeni sasa iwaje ashikwe na tamaa ya kutaka
kushika madaraka ya juu .
Hata
hivyo, alisema atagombea tena nafasi hiyo kupitia Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT), ili wanawake wampe tena kura zao kwani anajijua bado
anafaa zaidi ya kufaa, hivyo atajitokeza katika uchaguzi mkuu ujao wa
2015 kutetea nafasi yake hiyo kwa tiketi ya Chama cha mapinduzi..
|
No comments:
Post a Comment