Wanafunzi waliohitimu Alphabeta Music Centre, Tabata |
Asilimia
kubwa ya wanamuziki hapa Tanzania wanapiga muziki bila ya kuwa na elimu yoyote
ya awali ya muziki. Viongozi wengi wa nchi wamekuwa wakitoa kauli nzuri za
kusifu sanaa hii na wasanii wa sanaa hii lakini ni nadra kusikia kiongozi
akiongelea matayarisho rasmi katika sanaa hii, na kwa ukweli hata katika sanaa
nyingine.
Kama
ambavyo kumekuweko na kufa kwa viwanda nchini humu ndivyo ilivyotokea katika elimu
ya sanaa. Zamani sanaa ilianza kufundishwa kuanzia darasa la kwanza, na hata
syllabus ya elimu hiyo mpaka leo ipo, ila haitumiki. Vyuo, kama Chuo cha
Waalimu Butimba kule Mwanza, kilitoa waalimu ambao walikuwa maalumu kwa ajili
ya kufundisha sanaa katika shule zetu kuanzia shule za msingi, bahati mbaya
sana haya yote yametupwa uvunguni, hivyo Taifa linakwenda kihobelahobela katika
tasnia ya sanaa. Kuna vyuo, kwa mfano Chuo cha Sanaa Bagamoyo, ambacho hupokea
wanafunzi kwa ajili ya kupata elimu ya sanaa, lakini utaona wazi kwa kuwa
hakuna mtiririko wa elimu hiyo kutokea shule za msingi, elimu hiyo ina
walakini. Na zaidi katika ngazi ya Chuo Kikuu, mtu anapata digrii baada ya
kusoma miaka mitatu bila ya kuwa
na elimu ya awali inayoonyesha mtu huyu alikuwa na vyeti gani vya msingi katika
taaluma yake.
Utafiti
umeonyesha kuwa kupata elimu ya muziki kuanzia umri mdogo kuna faida nyingi
sana. Kwanza humuwezesha mtoto kukuza sehemu ya ubongo ambayo huhusika na lugha
na pia kukuza uwezo wake wa kutafakari. Inaeleweka kuwa ubongo huendelea kupata
maendeleo miaka mingi baada ya kuzaliwa, hivyo muziki huendeleza kuboresha
upande wa kushoto wa ubongo ambao ndio huhusika na ujuzi wa lugha na tafakari. Muziki husaidia sana watoto
kukumbuka mambo mbalimbali, ndio maana hata matangazo ya biashara ya kawaida
husindikizwa na muziki ili kukaa katika kumbukumbu kwa urahisi. Kwa watoto,
muziki husaidia sana katika kazi zao za elimu ya kila siku.
Wasanii
waliopata elimu sahihi huwa na uwezo wa kubuni majibu mbali mbali kwa tatizo
moja, hii unaweza kuiona kwa mfano ukiwapa wanamuziki kumi semina kuhusu jambo,
kwa mfano ukimwi kisha ukawambia watunge wimbo kuhusu elimu waliyopewa,
utashangaa watakuja na tungo tofauti za mtizamo mpya kabisa wa kuelezea elimu
hiyo waliyoipata. Elimu ya muziki hufungua ubongo
kuruhusu kuachana na mawazo mengi yaliyopita na kujaribu mawazo mapya.
Wasanii kote duniani huwa waanzilishi wa mambo mengi ikiwemo mitindo ya nguo,
uvaaji na mambo mengi katika maisha kutokana na ubongo wao kuwa na uwezo wa
kuruhusu kufikiria vitu katika mtazamo mpya. Elimu ya awali ya muziki
imeonyesha kuwa wanafunzi wa elimu hii hufanya vizuri zaidi katika masomo
mengine, tofauti sana na mawazo ya kawaida kuwa muziki huharibu watoto. Katika
muziki, kosa huwa ni kosa , ukikosea beat, usipotyuni chombo chako, ukiimba
vibaya ni kosa hakuna mbadala, sauti ikiwa juu mno, au chini mno nakadhalika,
na mwananmuziki hulazimika kurudia tena na tena mpaka atakapopata kitu sahihi
kabisa, elimu hii ikiwa kichwani kwa mtoto toka umri mdogo humsaidia katika
kuboresha mambo yake mengine na kuyafanya vizuri zaidi kila mara. Elimu ya
awali ya muziki humjenga mtoto kujua kufanya kazi na watu wengine kama kundi, kutokana
na kuelewa kuwa katika muziki watu wengi hutegemeana ili kuleta ubora katika
wimbo mmoja, hii huwasaidia katika maisha ya kila siku. Kuna mengi
yanayopatikana katika elimu bora ya sanaa, pia kubwa likiwa ni kwenda sambamba
kitaaluma na ulimwengu, kuna bahati mbaya sana kwa vijana wetu kutaka kuingia
katika soko la muziki duniani lakini bila kuwa na matayarisho yanayostahili
kufikia huko, wengi ndoto zao hazitatimia kwani elimu ya kufikia huko hawana.
Nilishaona hii makala kwenye blog fulani
ReplyDeleteNilishaona hii makala kwenye blog fulani
ReplyDelete