Simba Sports club imesikitishwa na
kitendo cha Young Africans kuvunja taratibu za usajili kwa kumrubuni mchezaji
wake Kelvin Patric Yondani kwa
kuzungumza naye na baadae kwa ushahidi wa picha kuonekana wakimuandikisha
makaratasi ambayo baadae imeripotiwa na vyombo vya Habari kwamba alikuwa akisaini
mkataba wa kuichezea timu hiyo ya Young Africans.
Kwamba katika picha hiyo ameonekana
mjumbe wa Young aliyejiuzuru bwana Seif Ahmed na hilo lilitoa shaka kama
utaratibu huo umefanywa na klabu ya Young, lakini shaka hiyo imeondolewa pale
ambapo tovuti ya Young imetangaza kumsajili mchezaji huyo wa Simba SC, lakini
zaidi ya hilo picha inaonyesha fedha zikiwa zimewekwa mbele ya mchezaji jambo
linaloonyesha mazingira ya kurubuniwa kwani kwa utaratibu wa kifedha, pesa
nyingi kiasi hicho malipo yake yanashauriwa/yanapashwa kupitia benki.
Mbali ya hayo picha hiyo inamuonyesha
Kelvin akiwa katika jezi ya mazoezi ya timu ya Taifa na yenye logo ya
Kilimanjaro na kumbukumbu zinaonyesha mkataba kati ya TBL na TFF tarehe 9/5/2012,
kwa haraka haraka tukio hilo limefanyika katika kipindi chini ya mwezi mmoja
ingawa taarifa za ushahidi zinaonyesha tukio hilo limetokea jana tarehe 6/6/2012.
Simba Sports Club ilipenda kuamini kwamba
tukio hilo haliihusu klabu ya Young kwani bwana Seif Ahmed alishajiuzuru kutoka
kwenye kamati ya Young Africans, kwani Young ni klabu kongwe na inayojua
taratibu zote za usajili.
Kwamba Simba Sports Club imeshawasiliana
na jopo lake la mawakili na inajiandaa kuishtaki klabu ya Young katika chombo
husika cha mpira na kudai adhabu ya kutopitisha majina yote ya usajili ya Young
kwa mwaka 2012/2013 na miaka mingine miwili ijayo na Simba SC ipo tiyari
kufuatilia suala hili hadi katika mahakama ya mpira ya FIFA.
Kelvin Yondani ni mchezaji halali wa
Simba Sc aliye na mkataba hadi 31 mei 2014 mkataba ulioongezwa tarehe
23/12/2011 kuundeleza mkataba wa awali uliokuwa unaisha tarehe 31/5/2012.
Sheria za FIFA za hadhi na uhamisho wa wachezaji ziko wazi katika kipengele cha 5 kifungu kidogo cha 2
kinasema kwamba mchezaji atasajiliwa kuichezea timu moja tu kwa wakati mmoja.
Imetolewa leo tarehe 7/6/2012.
MH. ISMAIL ADEN RAGE (MB)
MWENYEKITI
SIMBA SPORTS CLUB
No comments:
Post a Comment