STRAIKA Donald Ngoma wa FC Platinum ya Zimbabwe alitarajiwa kutua nchini jioni ya leo na ilitarajiwa jioni ya kesho angeishuhudia Yanga inayotaka kumsajili ikitambulisha nyota wake wapya katika pambano dhidi ya Sc Villa ya Uganda.
Hata hivyo mchezaji huyo imeshindikana kutua leo, lakini hakuna kilichoharibika kwani Yanga itatambulisha nyota wake wote mbele ya Waziri Mkuu na Mtangaza Nia ya Urais, Mhe. Mizengo Pinda. Waziri Pinda atakuwepo katika pambano hilo ili kubariki silaha hizo mpya za Jangwani wakati wa mchezo huo maalum wa kuchangisha fedha za Ujenzi wa Majengo ya Watoto Wanaoisha katika Mazingira Magumu.
MKurugenzi wa asasi wa Nyumbani Kwanza, Mossy Magere aliiambia MICHARAZO MITUPU kuwa, Yanga itavaana na SC Villa ambapo pia kutakuwa na burudani ya kutosha kwa watakaohudhuria.
Mossy alisema kuwa, Waziri Pinda ndiye mgeni rasmi katika pambano hilo ambalo Yanga watalitumia kutambulisha nyota wake wapya na kusindikizwa na burudani ya muziki toka kwa kundi la Yamoto Band.
"Maandalizi yamekamilika na kwamba wageni mbalimbali tumewaalika, ila Waziri Pinda ndiye atakayekuwa mgeni rasmi na atabariki kikosi hicho cha kocha Hans Pluijm," alisema Mosi.
Mosi alisema kuwa SC Villa walitua juzi jioni wakiwa na kikosi cha wachezaji 18 na viongozi watano na kwamba jana walipasha misuli kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya leo kuivaa Yanga.
Yanga ambao imetoka kuichapa Friends Rangers kwa mabao 3-2 katika mechi ya mazoezi, inauchukuliwa kwa uzito mkubwa mchezo huo wa leo kwani ni sehemu ya maandalizi ya ushiriki wao wa michuano ya Kagame na kocha atataka kupima uwezo wa wachezaji wao mbele ya Villa.
Baadhi ya wachezaji wapya wa Yanga ambao watakuwa majaribuni ni Malimi Busungu, Geofrey Mwashiuya na kipa Benedict Tinocco kwani Mwinyi Haji Ngwali na Deus Kaseke wapo kambi ya Taifa Stars kujiandaa na pambano la marudiano la kuwania Chan dhidi ya Uganda The Cranes.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alinukuliwa juzi kuwa, huenda akawashtukiza mashabiki wa klabu hiyo katika mchezo huo wa kesho, bila kufafanua lakini imebainika ni kwamba Donald Ngoma alipangwa kuwepo uwanjani kuwashuhudia wenzake kwani angetua nchini ili kumalizana na klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment