Mwandishi wetu
KILA mwanadamu anapoamua kufanya kazi ya aina fulani lengo na
hitaji lake ni kuhakikisha anapata mafanikio yatakayomuwezesha
kuendesha maisha yake kama watu wengine.
Hivyo ili kufikia mafanikio hayo nidhamu, upendo, elimu na
kujitabua ni mambo ambayo yanahitajika kuhakikisha malengo
yanafikiwa kwa asilimia mia moja.
Kwa maana nidhamu ikizingatiwa kuanzia katika mazoezi hadi
kwenye ulingo hakika kila kitu kitakwenda sawa na hakika hiyo ndio
mwanzo wa kufanikiwa katika mchezo huo.
Ndio maana kwa mabondia walioanzia katika hatua za awali
'Amature' mara zote wanakuwa na nidhamu kubwa katika maisha yao
katika mchezo huo na kuwa mfano kwa wengine.
Kitendo cha kufanya vema katika nidhamu ndio inayofanya viongozi
wa mchezo huo kuhamasisha vijana wanaotaka kuingia katika
masumbwi kuanzia kwenye hatua hiyo.
Pindi bondia atakuwa na nidhamu ya kutosha itafanya kuhamasisha
upendo katika familia ya wanamasumbwi nchi na upo uwezekano
mabondia wakawa wamoja katika kufuatilia mambo yao.
Katika kipindi cha hivi karibuni mchezo wa masumbwi unaonekana
kupoteza radha yake kutokana na kuonekana kuwa kuingiliwa na
baadhi ya wajanja ambao wanaonekana kutaka kuwagawa
wanamasumbwi.
Wajanja hao wamekuja na vyama vyao na kujipa majina ya kila aina
likiwemo la urais wa chombo husika huku wakionekana wazi
kutafuta maslahi yao zaidi kuliko wanamasumbwi ambao wamekuwa
wakiharibu akili zao kwa ajili ya mchezo huo huku mafanikio yakiwa
kiduchu.
Kibaya zaidi hakuna chombo makini cha kuangalia na kufuatilia haki
za wanamasumbwi, kingine wanamasumbwi wengi elimu na ufahamu
wa kudai haki yao imekuwa ni tatizo hali ambayo inasababisha
mabondia kugonganishwa vichwa na wanaojihita marais wa vyombo
hivyo.
karibuni mwaka huu wakati nikiwa katika daladala nikitokea nyumbani
kwenda ofisini, kituo kimoja cha redio kilikuwa kikifanya mahojiano
na bondia Japhet Kaseba majiahano ambao yalionekana kurekodiwa
siku chache zilizopita.
Hakika Kaseba alisikika akizungumza kwa uchungu namna baadhi ya
mabondia wanavyotumiwa vibaya na baadhi ya viongozi huku
akisema wengi wamekuwa wakipandikizwa chuki dhidi ya mabondia
wengine.
Pia wako tayari kufanya hila ili kutengenezewa rekodi ya mapambano
pindi wanapopanda ulingo hali ambayo mwisho wa siku wanafanya
vibaya katika mapambano yao ya kimataifa na ndipo msemo wa
kiswahili unaosema mwisho wa ubaya ni aibu unapotimia.
Nikinukuu katika mazungumzo hayo, Kaseba anasema kuwa baadhi
ya mabondia wanatumika vibaya kwa kujazwa chuki na wakati
mwingine kwa kupanga matokeo kutokana na shida walizonazo.
Pia hata wale ambao haki zao zinaminywa wanashindwa kujitetea
kutokana na elimu yao kuwa ndogo ingawa hakuweza kutoa
suluhisho ya nini kifanyike ili kuondokana na changamoto hiyo.
Kwa akili ya haraka ni dhahiri kuwa kinachotakiwa ni kwamba kwa
sasa ni kila bondia kutambua ameingia katika mchezo huo kwa ajili
gani hali ambayo itasaidia kupunguza changamoto kwa baadhi yao
kuwa mamluki wa viongozi wa baadhi ya vyama.
Pia itasaidia mabondia kuwa kitu kimoja katika kusaka mafanikio yao
kupitia mchezo huo unaonekana kuwa na changamoto lukuki hali
ambayo inaonekana kupoteza radha na mafanikio yaliyokuwa
yakipatikana miaka kadhaa iliyopita.
Kinachotakiwa kwa sasa ni mabondia kujitahidi kuwa kitu kimoja hali
ambayo itasaidia kuwa na nguvu moja ya kudai haki zao pindi
zinapopindishwa kwa maslahi ya wengine