Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, April 16, 2016

HAKUNA MUDA WA KULALA, WAZIRI MKUU AIAMBIA DART

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaambia watendaji na wadau wa mradi Mabasi Yaendayo Haraka wa jijini Dar es Salaam (BRT) kuwa hawana muda wa kulala wa kupumzika na akawataka wakamilisha haraka vipengele vichache vilivyobakia ili mradi huo uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo. 

Ametoa agizo hilo jana usiku (Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam. 

“Watu wa DART, UDA-RT hakuna muda wa kulala tena. Nanyi wa eGA, MAXCOM, POLISI NA SUMATRA inabidi mfanye kazi kama timu moja na wenzenu ili maeneo yaliyobakia yaweze kukamilika katika muda mfupi na kikubwa ni kuhakikisha mnatoa elimu ya kutosha,” alisisitiza. 

Akielezea utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Ronald Rwakatare amesema miundombinu ya mradi huo imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani hivi sasa wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji nauli na uendeshaji wa mabasi hayo. Pia aliwatka wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo na kuwa makini na matumizi ya barabara wakati mradi huo ukiwa kwenye majaribio na hatimaye kuanza kazi rasmi. 

Alisema watakuwa na karakana itakayotumika kwa ajili ya hayo mabasi ambayo itakuwepo eneo la Jangwani na kwamba ofisi za mradi pia zitakuwa eneo hilo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw. Robert Kisena amesema mpango wa kuanza kwa mradi huo umekamilila na tayari mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja na bima. UDA-RT ni kampuni ya muunganiko wa UDA na wamiliki wa daladala ya kutoa huduma ya usafiri katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka. 

Bw. Kisena amesema kesho wataanza majaribio ya mradi huo kwa kutumia mabasi 10 na watakuwa wanaongeza mabasi 10 kila siku hadi yafikie 50 hivyo amewataka wananchi kuondoa shaka juu ya mradi huo. Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Maxcom Africa, Bw. Juma Rajab amesema mabasi hayo yatakuwa yanatumia kadi za kielektroniki zitakazokuwa zinalipiwa kwa kutumia mitandao mbalimbali ya simu za mkononi. 

Bw. Rajab amesema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba fedha za mteja zitakuwa salama na hata kama atakapopoteza kadi yake. “Mtu akinunua kadi yake anapaswa atunze namba ya usajili iliyoko kwenye kadi hiyo kwani itatumika kurudishia fedha zake kupitia namba yake ya simu ya mkononi,” alisema. 

Amesema Maxcom Africa ndio wakusanyaji wa nauli kwa kushirikiana na UDA-RT ambapo watatumia mawakala wa MaxMalipo hivyo kila mwananchi atapata fursa ya kununua kadi yake kwa urahisi. Alisema taarifa za kila mtumiaji zitaunganishwa na simu yake ya mkononi ambapo mhusika ataweza kujua kwa urahisi salio la fedha lililomo kwenye kadi yake. 


IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU 
2 MTAA WA MAGOGONI, 
S. L. P. 3021, 
11410 DAR ES SALAAM 
JUMAMOSI, APRILI 16, 2016.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...