Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, December 31, 2016

CHEKA AFUNGIWA MIAKA MIWILI NA TPBC KWA KUMKIMBIA DULLA MBABE



Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Chaurembo Palasa akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam,  kuhusu bondia Francis Cheka ambaye amefungiwa miaka miwili pamoja na kulipa faini ya Shilingi 500,000. Kulia ni Mwenyekiti Kamati ya Ufundi TPBC, Ally Bakari na katikati Katibu Msaidizi wa TPBC, Mchatta Michael

KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), imemfungia bondia Francis Cheka kujihusisha na ngumi kwa miaka miwili pamoja na faini ya Sh 500,000 ikiwa ni siku moja tangu bondia huyo  atangaze kustaafu.

Juzi Cheka alitangaza kustaafu kucheza ngumi akidai kwa muda mrefu amekuwa akipigana bila mafanikio kutokana na kudhulumiwa na waandaaji wa mapambano au kulipwa tofauti na makubaliano pamoja na misukosuko anayofanyiwa na wapinzani wake.

Cheka ilikuwa apande ulingoni Desemba 25 mwaka huu kupigana na Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ lakini hakufanya hivyo akidai kumaliziwa kwanza fedha zake.

Pambano hilo liliandaliwa na bondia Siraji Kaike. Mwanzoni mwa wiki hii bondia huyo alikamatwa na Polisi Morogoro kwa kosa hilo la kuchukua nusu ya fedha na kutopanda ulingoni ambapo alishikiliwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa.

Akizungumza na wandishi wa habari jana, Rais wa TPBC Chaurembo Palasa, alisema Cheka amefungiwa kutokana na  kutofika ulingoni kwenye pambano hilo la siku ya Krismasi.

“Cheka aliingia makubaliano na promota Siraji Kaike ya kupigana na Dulla Mbabe, lakini hakufika kwenye pambano jambo ambalo halileti picha nzuri kwenye ngumi za kulipwa hivyo tumemfungia pamoja na faini juu,” alisema Palasa.

Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari, Palasa aliongozana na Mwenyekiti Kamati ya Ufundi wa TPBC, Ally Bakari na Katibu Msaidizi wa kamisheni hiyo Mchatta Michael ambao walilaani kitendo cha Cheka kutopanda ulingoni kwani kilisababisha promota Kaike kupata hasara na pia kinarudisha nyuma ngumi kwani wanaonekana wababaishaji.

Kwa mujibu wa Cheka, alipaswa kulipwa Sh milioni tisa, lakini hadi wakati wa kupima uzito alikuwa amepewa Sh milioni tatu pekee ndio maana hakupima uzito kwani kisheria ukipima uzito umekubali kucheza.

Baada ya kutangaza kustaafu Cheka amesema anajielekeza kufanya biashara zake na ameahidi ushirikiano kwenye mchezo wa ngumi ili kukuza na kuendeleza mchezo.

Akizungumzia kufungiwa kwake Cheka alisema hatambui maana yeye si mwanachama wa TPBC.

“Bondia wa kulipwa hana chama wala mwanachama, kuna mkataba walifoji (kughushi) saini yangu waliuona? au wanahukumu upande mmoja, kwa nini wasinitafute wakanisikiliza na mimi? Mimi nadhani sasa viongozi waende wakosomee uongozi, serikali itusaidie hili,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...