Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, August 1, 2011

DEWJI AWAHIMIZA WALIMU JIMBONI MWAKE KUFANYAKAZI KWA BIDII ILI KUONDOA AIBU YA MATOKEO YA MITIHANI.


Na.Mwandishi wetu.

Walimu wa shule za sekondari jimbo la Singida mjini, wamehimizwa kukaza ‘buti’ katika kutekeleza wajibu wao, ili kuinua taaluma itakayowawezesha wanafunzi kuondokana na aibu ya matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha pili na ule wa kidato cha nne.

Changamoto hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na mbunge wa jimbo hilo, Mohammed Gullam Dewji, wakati akizungumza kwenye kikao cha pamoja na walimu wa shule 20 za sekondari za manispaa ya Singida.

Aliwaomba waendelee na moyo wao huo wa kujituma kwenye kazi yao ya ufundishaji, ili kunyanyua ufaulu wa wanafunzi.

“Taarifa nilizo nazo, hali ya ufaulu kwenye shule zetu iko chini mno, ni imani yangu kuwa baada ya kikao chetu hiki, morari na juhudi za ufundishaji mtaziendeleza kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi” alifafanua.

Aidha, Dewji ambaye pia ni mjumbe wa MNEC wa mkoa wa Singida,aliwataka waendelee kuwa wavumilivu wakati huu ambao serikali inaendelea kutatua changamoto nyingi zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Changamoto mlizoziwasilisha kwangu, tutajipanga mimi na viongozi wenzangu tuone ni kwa jinsi gani tunaweza kuzitatua zile zilizo ndani ya uwezo wetu, na zile ambazo ziko nje ya uwezo wetu, tutaziwalisha serikalini kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kudumu”,alisema.

Awali afisa elimu wa shule za sekondari katika manispaa ya Singida, Magreth Mafita, alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili ofisi yake, kuwa ni kucheleweshwa kulipwa kwa madai ya walimu na uhaba mkubwa wa walimu.

Mafita alitaja changamoto zingine kuwa ni uhaba wa vyumba vya madarasa, shule mpya kutokuwa na barabara za kuziunganisha na sehemu zingine na ufaulu usioridhisha wa asilimia 42.

“Hata hivyo, mheshimiwa mbunge naomba nitumie fursa hii kukupongeza sana kwa juhudi zako za dhati zilizopelekea jimbo la Singida mjini, kuwa na shule za sekondari za serikali 17 kati ya mbili zilizokuwepo mwaka 2005”,alisema afisa huyo na kushangiliwa kwa nguvu na umati wa walimu.

fullshangwe.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...