Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, November 16, 2015

MJUWE BONDIA LULU KAYAGE ANAETAMBA KATIKA ANGA ZA KIMATAIFA

Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' akimnowa bondia Lulu Kayage wakati wa mazoezi yake ya kujiandaa na mpambano wake wa kugombania mkanda wa taifa desemba 25 na bondia Mwanne Haji mpambano utakaofanyika mkoa wa Morogoro katika uwanja wa jamuhuri picha na SUPER D BOXING NEWS



BONDIA LULU KAYAGE

 Katika kipindi cha hivi karibuni wamewika mabondia wengi sana nchini lakini kwa sasa mabondia wanaotamba na kufanya vizuri wana hesabika ukiondoa kwa upande wa wanaume bondia anaekuja juu zaidi kwa sasa kwa upande wa wanawake ni Lulu Kayage 

 
akizungumza na mwandishi wa makala haya 
bondia huyo kwa ajili ya kuelezea maisha yake  nje ya ulingo. Yafuatayo ni mahojiano hayo:
 mwandishi, Unajihusisha na mchezo  wa ngumi ambao wengi wanaona ni wa kiume, je kama msichana ni changamoto gani unakumbana nazo katika maisha?
Lulu: Kwa kawaida unapokuwa kwenye mchezo wa masumbwi  mtaani watu wengi wanakuogopa wanakuchukulia   kama mgomvi muda wowote unaweza  kupigana na mtu lakini ni tofauti  kwa sababu ukishaingia huku hupigani hovyo.  Changamoto nyingine mimi  nikiongea  sauti yangu  ya asili ni kubwa hivyo ninapokuwa kwenye biashara zangu mtu anaweza akaja kununua kitu nikimjibu anaona naongea kwa hasira wakati sio hivyo.
 mwandishi: Ni kweli huwa mnakuwa wababe na wewe uliwahi kupigana  na mtu mtaani huku ukiwa bondia?
Lulu: Zamani nilikuwa napenda ugomvi  na mtu akinichoza nampiga kweli  lakini  tangu  nimeanza mazoezi ya ngumi hali hiyo iliondoka na kama kupigana najisikia raha nikiwa ulingoni ni kupigana  na bondia mwenzangu. Hata sasa akitokea  mtu aseme tupigane hadharani  tofauti na mchezo naogopa na ninaweza kupigwa  kwa kuwa nitapigana kwa hofu ya kuwa  ninayepigana naye nitamuumiza endapo  nitampiga sehemu mbaya kwa sababu uwezo wa kunipiga hana.
mwandishi: Familia inachukuliaje kazi unayofanya ya kupigana ngumi  na wewe ni mtoto wa kike?
Lulu: Wamepokea vizuri tu na wananiaunga mkono kwa sasa lakini nilivyoanza niliwaficha na walifahamu kuwa nacheza ngumi baada ya kuona picha yangu kwenye gazeti  napigana  wakashangaa na  kuniuliza imekuwaje  nimeingia huko wakati wanajua mimi nafanya riadha.
mwandishi: Kama watu wanakuogopa rafiki zako  wa karibu ni kina nani?
Lulu:Mimi marafiki zangu ni watoto wa kiume kwa bahati mbaya au nzuri sina rafiki wa kike, ukiniona nimeongozana na msichana ujue ndugu yangu. Sina mazoea na wasichana tangu nilipokuwa shuleni.
mwandishi: Kwa nini hupendi kuwa na marafiki wa kike?
Lulu: Wanawake mara nyingi wanakuwa na midomo  ya kuzungumza mambo ya watu yasiyowahusu sasa mimi sipendi. Hata  nyumba niliyopanga wanajua kama rafiki zangu wanaofika nyumbani kwangu ni wavulana. Imefikia hadi wasichana wenyewe wanashindwa kunizoea hawajui  waanzie wapi  kuwa na urafiki na mimi  kwa sababu mambo ya kujadili watu siayapendi  lakini nikiwaona mahali wamekaa nawasalimia kama kawaida.
mwandishi: Kuna vitu vingine  katika maisha lazima umshirkishe msichana mwenzako,  huwa unafanyaje wakati watu wako wa karibu wavulana?
Lulu: Nikihitaji  ushauri au vitu vinavyohusu msichana huwa nawashirikisha wasichana ambao ni ndugu zangu.
mwandishi: Mara nyingi mavazi yako huwa kama ya kiume, je hiyo inatokana na  unavyokaa  karibu nao?
Lulu: Nahisi hivyo kwa sababu  siku nikivaa gauni sijui kuna nini sio rahisi. Lakini Kikubwa  kilichochangia  kupenda mavazi haya ni kwa sababu nimelelewa na baba  tangu nikiwa na miezi mitano baada ya mama yangu kufariki. Unajua  mwanaume anavyolea mtoto huwa hamvalishi sketi kutokana na mazingira na ikawa nikivalishwa sketi nalia kutwa nzima  hata nilivyoanza  shule nguo niliyoshonewa juu sketi ndani imetengenezwa kama suluari
mwandishi: Umeolewa, una mchumba au unaishi na nani?
Lulu: Sijaolewa na wala sina mchumba, ninaishi mwenyewe.
mwandishi: Kwa nini au ndio  hivyo wanakuogopa?
Lulu: Nadhani muda bado haujafika na wapo wanaonifuata nakataa kwa sababu  wengi ni vijana ambao siwaelewi kwa kuwa haiwezekani mtu aje amevaa suluari mlegezo halafu nimkubali. Mimi navaa suluari lakini sipendi mtu anaevaa mlegezo.
mwandishi: Maisha ya kuishi msichana peke yake yana changamoto gani?
Lulu: Binafsi nayaona ni mazuri kwa kuwa napenda kujishughulisha na kazi. Nilikuja mjini nikiwa mdogo nikitokea Iringa na kufanya kazi za ndani kwa miaka miwili bila malipo.
mwandishi: Uliwezaje kufanya kazi bila malipo na ulikuja kulipwa fedha zako baadaye?
Lulu: Nilikuja kuondoka, bahati nzuri mama niliyekuwa naishi naye alikua anafuga ng’ombe  akawa ananipa maziwa nauza hivyo nikawa napata hela kidogo  ambazo nabakisha sokoni  nikafungua akaunti benki nikawa naweka hadi  nikafikisha 600,000 nikaondoka  nikatafuta chumba. Kutokana na utoto nilipata shida kupata kwa kuwa kila ninapokwenda kwa mwenye nyumba ananikataa hadi  nikatafuta msaada polisi wakaniasaidia.
mwandishi: Ilikuwaje ukaingia kwenye ngumi?
Lulu: Ni mchezo niliokuwa naupenda, kwa kuwa nilikuwa nafanya mazoezi ya riadha nikakutana na kijana mmoja  anaitwa Omari Bai nikamuuliza  wapi wanafundisha ngumi akanipeleka kwa mzee Habibu Kinyogoli 'Masta'.
mwandishi: Unafanya mazoezi mara ngapi kwa siku?
Lulu: Mazoezi nafanya mara mbili.
mwandishi: Unapendelea chakula gani?
Lulu: Napenda ugali maharage na mboga za majani na asubuhi napendelea kula matunda.
mwandishi: Kitu gani kinakuongezea kipato?
Lulu: Nafanya biashara ya matunda. Nina genge langu la kuuza matunda lipo maeneo ya  Mkwajuni, Kinondoni.
mwandishi: Kuna  vishawishi vingi kwa vijana kama vile matumizi ya dawa za kulevya  hasa ukiwa kwenye michezo, wewe unajizuaje?
Lulu: Namshukuru Mungu malezi ya baba yamenilinda kwa kuwa sijawahi kumuona akivuta sigara, kunywa pombe au kuingiza mwanamke ndani  hivyo ni ngumu mimi kufanya vitu hivyo. Nikiwa na rafiki anatumia vitu hivyo naepukana naye.
Bondia huyo kwa sasa anasimamiwa mapambano yake ya ndani na nje ya nchi na kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa mchezo wa masumbwi nchinin 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...