BENDI ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ itatumbuiza kwenye bonanza la vyombo vya habari litakalofanyika Jumamosi wiki hii Coco Beach, Dar es Salaam.
Pia Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kitatumia bonanza hilo kutoa tuzo maalum kwa waandishi wa habari ambao hivi sasa wamepata nafasi katika vyama vya michezo ama taasisi nyingine mbalimbali kubwa za kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema maandalizi ya bonanza hilo litakalohudhuriwa na watu 1000, kati yao 800 wakiwa ni kutoka vyombo mbalimbalimbali vya habari yanaenda vizuri.
Alisema bonanza litaanza saa nne asubuhi hadi saa mbili usiku na kwamba vyombo mbalimbali vya habari vimealikwa na kuwa kila chombo kinatakiwa kuthibitisha michezo kitakayoshiriki kwa Katibu Mkuu wa TASWA kabla ya Alhamisi saa tano asubuhi ili ratiba ipangwe.
Alisema michezo mbalimbali itashindaniwa ambayo ni soka ya ufukweni (wanaume), netiboli (wanawake), wavu (jinsia zote watachanganyika), mbio za magunia (wanawake na wanaume), mbio meta 100, kuruka kichura (wanawake na wanaume) na kuvuta kamba (jinsia zote watachanganyika) na kucheza muziki (wanawake na wanaume).
Alisema michezo yote itakuwa na zawadi ya vikombe isipokuwa kucheza muziki zawadi yake ni fedha taslimu, ambayo itatangazwa Alhamisi.
Kuhusiana na tuzo, Pinto alisema Kamati ya Utendaji ya TASWA imekubaliana kuwa wapo waandishi ambao wamepata nafasi mbalimbali kwenye taasisi tofauti, lakini kwa kutambua mchango wao, TASWA imeamua kuwapa tuzo.
“Idadi yao ni kubwa sana, lakini tumeamua kwa vile sisi tuliingia madarakani Agosti mwaka jana, basi waandishi wote ambao wapo kwenye taasisi nyingine, lakini walikuwa waandishi wa habari mpaka wanapata nafasi hizo tutawapa tuzo.
“Mfano ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, Wabunge Lucy Mayenga, Juma Nkamia, Esther Bulaya na wengine wengi.
“Nitoe angalizo kuwa tunawapa tuzo maalum ambayo itaonekana siku hiyo wale waliopata mafanikio hayo kuanzia Agosti mwaka jana, orodha kamili tutaitoa Alhamisi kwenye mkutano wetu na wana habari.
“Si waandishi wa michezo tu, bali hata wa siasa, uchumi na mambo mengine, lakini wawe katika vyama ama taasisi za kitaifa, si klabu ama taasisi ndogondogo,” alisema Pinto.
Naye Meneja Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambao ndio wadhamini wa bonanza hilo, Edith Mushi alisema udhamini wao unagharimu kiasi cha sh. Milioni 50 na kuwa kampuni yake na TASWA zimegawana majukumu kwa bonanza hilo.
Jana TBL ilikabidhi mfano wa hundi y ash. Milioni nane, ambayo TASWA ndiyo itayashughulikia kwa ajili ya bonanza hilo, huku mengine ikiwemo masuala ya vinywaji yakifanywa na TBL.
“Kama mnavyofahamu TBL imekuwa karibu na waandishi wa habari katika masuala mbalimbali na ndiyo sababu imeweka nguvu zake kwenye bonanza la mwaka huu.
“TBL itahakikisha bonanza la mwaka huu linafana na linakuwa la aina yake kuanzia katika michezo, vinywaji na vyakula ili kila mmoja aamini kwamba kweli limedhaminiwa na kampuni ya vinywaji.
“Tunawaomba waandishi wajitokeze kwa wingi huku tukiamini kwamba kila mmoja atafurahi siku hiyo, maana lengo ni kuwakutanisha pamoja watu wa tasnia hii na kubadilishana mawazo na pia kupongezana kwa kazi ngumu mnayoifanya,” alisema
Naye Meneja wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Hassan Rehani alisema bendi yake ipo imara na kuwa waandishi watakaofika siku hiyo watafurahi zaidi.
No comments:
Post a Comment