Mwenyekiti
wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage akizungumza na Waandishi wa Habari
jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya klabu hiyo katika Mikoa ya Kanda
ya Ziwa. (Na Mpiga Picha wa Habari Mseto Blog).
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe akifafanua jambo wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari.
DAR ES SALAAM, Tanzania
MABINGWA
wa ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara timu ya Simba kwa kushirikiana na
mdhamini wa klabu hiyo Kampuni ya Bia nchini (TBL), leo wametangaza
muendelezo wa sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kufanya ziara
katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyoratibiwa na Nationwide
Entertainment Center, yenye Makao Makuu Posta Road jijini Mwanza.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa TBL Ilala, Dar es
Salaam, Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alisema kuwa, ziara ya
mabingwa hao kanda ya ziwa itakuwa ya siku mbili Juni 16 na 17,
ikihusisha mechi mbili za kirafiki ikiwamo dhidi ya Toto Africans –
ambayo itatumika kuipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa na Toto kwa kubaki
Ligi Kuu Bara.
“Tutatoka
jijini Juni 15 kwa ndege na Jumamosi Juni 16 tutacheza mechi dhidi ya
Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, kabla ya Juni
17 kushuka CCM Kirumba Mwanza kuumana na moja ya klabu kutoka nchini
Uganda, ambayo tutawaarifu baada ya kukamilika kwa makubaliano muhimu,”
alisema Rage.
Rage
aliongeza kuwa, katika ziara hiyo Simba itakuwa na kikosi chake kamili
kinachotarajia kucheza Kombe la Kagame, wakiwamo nyota wapya na wa
zamani, kutoka ndani na nje ya nchi. Akabainisha kuwa, muda ukiruhusu
kabla ya kuanza kwa Kagame, watasafiri mikoa ya Lindi na Mtwara kwa
ziara kama hiyo.
“Kikosi
kitakachosafiri na hatimaye kucheza Kombe la Kagame, kitakuwa chini ya
kocha Milovan Cirkovic ambaye yuko likizo Serbia. Licha ya kumaliza
mkataba wake, Milovan atarudi nchini kuendelea na kazi na kama itatokea
tukashindwa kumaliazana naye, tutasema na kujua nani ataongoza kikosi”
alifichua Rage.
Kwa
upande wake Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alirudia
kuipongeza Simba kwa niaba ya TBL kwa mafanikio yao msimu ulioisha,
huku akisema: “Kama wadhamini, tuliziahidi Simba na Yanga mabasi mapya
ya wachezaji. Simba itakabidhiwa basi lao siku ya sikukuu yao ‘Simba
Day’ inayofanyika Agosti 8, lakini tutaangalia kama Yanga wao
watakabidhiwa lini,” alisema Kavishe.
Aliongeza
kuwa, kwa kutwaa ubingwa wa bara, Simba itapokea kutoka TBL kiasi cha
shilingi mil 25 kama mkataba unavyosema, ambapo Yanga kwa kushika
nafasi ya tatu, imepoteza kiasi cha shilingi milioni 15 ambazo ingepata
kama ingeshika nafasi ya pili nyuma ya Simba, ambayo hata hivyo
imeshikwa na Azam FC.
No comments:
Post a Comment