Mkuu wa Masista Waabuduo Damu ya
Kristo, Euprasia Julius akimtambulisha mgeni rasmi na meza kuu kwa
wageni waalikwa na wanakijiji wa Vikawe (hawapo pichani) katika hafla ya
ufunguzi wa Zahanati ya Da.Ma Africa Maria De Mathias (MDM) Vikawe,
Kibaha.
Na Mwandishi wetu, Kibaha
MGANGA Mkuu wa halmashauri ya Mji
Kibaha, Dk. Happniness Ndosi amepongeza shirika la masisita wa Waabuduo
Damu ya Kristo kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati ya kisasa katika
kijiji cha Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Mganga huyo ambaye alikuwa mgeni
rasmi katika hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo,pamoja na kuwapongeza
amesema serikali itaendelea kushirikiana na mashirika yote kwa lengo la
kuwezesha kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata kituo na kila wilaya
kuwa na hospitali.
Aliwapongeza masista hao kwa
kuonesha upendo na huruma kama Biblia inavyomsimulia msamaria mwema
ambaye alikuta mtu aliyepigwa na majambazi na kumsaidia.
Aliahidi ushirikiano wa serikali
katika kufanikisha usajili wa zahanati hiyo na kuendelea kuisaidia hatua
kwa hatua hadi inakuwa kituo mpaka watakapofanikisha safari yao ya kuwa
hospitali kubwa ya kisasa.
Mganga huyo pamoja na kutoa ahadi
hiyo aliwataka wananchi wa Vikawe kutumia huduma hiyo na kwamba zahanati
hiyo itakapohitaji msaada wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance)
wataletewa kuchukua mgonjwa na kumfikisha panapohusika.
Zahanati hiyo ya DA.MA Africa imejengwa kwa ufadhili wa wakristo wa Italia chini ya usimamizi wa Muitalia, Germano Frioni.
Akitoa salamu zake Muitalia huyo
amesema kwamba anawashukuru wakazi wa Vikawe kwa kumpa nguvu ya kusonga
mbele hasa kwa kutambua kwamba yeye na marafiki zake wamefanyakazi
usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia marafiki wa Afrika.
Alisema atajitahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha changamoto za zahanati hiyo zinafanyiwa kazi.
Aliwaomba wananchi wa Tanzania
kuendelea kumuombea yeye na wenzake kama Papa Francis anavyoagiza ili
malengo ya safari ya kuwapo duniani yafanikiwe.
Alisema kwamba watoto wake Daniel
na Marco (kwa sasa wote ni marehemu) ambao ndio kifupi cha zahanati hiyo
DA.MA wamemfanya kujitambua na kusaidia wengine katika kuonesha upendo.
Aidha alisema kwamba ataendelea
kukumbuka Vikawe kwani alifika mara ya kwanza mwaka 2005 na kuona hali
ilivyokuwa ambapo sasa lipo jengo la zahanati hiyo likiwa limekamilika.
Wazo la ujenzi wa zahanati hiyo ,
lilitolewa na wananchi wa Vikawe kwa Masisita Waabuduo Damu ya Kristo
mwaka 2004 wakati wakiwa katika eneo hilo baada ya kununua ekari 40 kwa
ajili ya kilimo mwaka 1994.
Alisema pamoja na maombi hayo na wao
wenyewe kutambua kwamba kuna mahitaji makubwa ya huduma ya afya
japokuwa kuna zahanati ya serikali, hawakuweza kutekeleza maombi ya
wanavijiji hadi mwaka 2011 walipofanikiwa kupata ufadhili kutoka Italia
na kuanza ujenzi mwaka 2013.
Katika risala yao walisema kwa
ushirikiano kati yao na wafadhili hao wamefanikiwa kuwapo kwa zahanati
hiyo yenye mahitaji yote ya msingi kwa mujibu wa taratibu za serikali na
kuzidi.
Msoma risala alisema kwamba wataendelea kupanua miundombinu mpaka zahanati hiyo ifikie ngazi ya cha afya na baadae hospitali.
Pamoja na ujenzi wa zahanati hiyo ya kisasa masisita hao wameanzisha shule ya awali kuwaandaa wanafunzi wa darasa la kwanza.
Wamesema kwamba wanaamini kwamba
wataendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa afya katika
kuimarisha huduma za hospitali hiyo.
Zahanati hiyo pamoja na vifaa tiba
pia ina raslimali ya visima vya maji ya mvua ujazo zenye ujazo wa lita
laki moja na kingine lita 49 elfu, wanatumia umeme wa sola na jenereta .
Walisema kwamba wanachangamoto ya kukosa umeme wa Tanesco, barabara nzuri na nyumba za wafanyakazi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Vikawe, Kibaha, Shabaan Mgini akiwasalimia wageni waalikwa wakati wa utambulisho.
Sr. Theresia Rogatus akisoma risala katika hafla ya ufunguzi wa Zahanati ya Da.Ma Africa DMD iliyopo Vikawe, Kibaha.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya
wilaya ya Kibaha, Dr. Happiness Ndosi akizungumza kwenye hafla ya
ufunguzi wa Zahanati ya Da.Ma Africa -DMD kijiji cha Vikawe, Kibaha.
Kutoka kushoto ni Mdau wa Zahanati hiyo, Dr. Zuberi Mzige wa Hospitali
ya Mwananyamala,
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya
wilaya ya Kibaha, Dr. Happiness Ndosi akimpa mkono wa shukrani Mfadhili
aliyejitolea kujenga Zahanati hiyo Raia wa Italia, Germano Frioni kwa
ujenzi wa Zahanati hiyo itakayohudumia wakazi wa kijiji cha Vikawe,
Kibaha.
Masista Waabuduo Damu ya Kristo
wakielekea meza kuu kwa mwendo wa madaha huku wakiwa wamebeba zawadi kwa
ajili ya kumkabidhi mgeni rasmi na wafadhili waliojitolea kujenga
Zahanati hiyo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya
wilaya ya Kibaha, Dr. Happiness Ndosi (kulia) akimkabidhi zawadi
Mfadhili aliyejitolea kujenga Zahanati hiyo Raia wa Italia, Germano
Frioni. Anaye shuhudia tukio hilo ni Baba Paroko wa Parokia ya Bikira
Maria wa Mlima Kalmeri Bunju...
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya
wilaya ya Kibaha, Dr. Happiness Ndosi akikabidhi zawadi kwa wadau
waliombatana na Mfadhili aliyejitolea kujenga Zahanati hiyo Muitalia,
Germano Frioni.
Mganga Mkuu wa halmashauri ya Mji
wa Kibaha, Dr. Happniness Ndosi (wa pili kulia) pamoja na Mfadhili wa
ujenzi wa Zahanati ya Da.Ma Africa ya kijiji cha Vikawe, Kibaha,
Muitalia, Germano Frioni wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa
Zahanati hiyo inayosimamiwa na Masista Waabuduo Damu ya Kristo nchini.
Muonekano wa ndani ya Zahanati ya Da. Ma Africa-DMD iliyop Vikawe, Kibaha mkoa wa Pwani.
Mganga Mkuu wa halmashauri ya Mji
wa Kibaha, Dr. Happniness Ndosi akiangalia chumba cha dawa katika
Zahanati hiyo mara baada ya kuzinduliwa.
Wageni waalikwa wakijadiliana jambo mara baada ya kufungiliwa rasmi Zahanati hiyo nje ya moja ya chumba cha upasuaji mdogo.
Baba Paroko wa Parokia ya Bikira
Maria wa Mlima Kalmeri Bunju akiendesha ibada takatifu ya misa maalum
kabla ya ufunguzi rasmi wa Zahanati hiyo.
Wanakijiji wa Vikawe wakishiriki ibada maalum wakati wa uzinduzi wa Zahanati ya Da. Ma Africa.
Kwaya ikitoa burudani.
Wageni waalikwa na wanakijiji wakishiriki kuimba pamoja na kwaya.
Pichani juu na chini ni baadhi ya wanakijiji na wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo.
Umati wa wageni waalikwa na wanakijiji wa Vikawe.
Mgeni rasmi Mganga Mkuu wa
Halmashauri ya wilaya ya Kibaha, Dr. Happiness Ndosi katika picha ya
pamoja na wadau pamoja na wafadhili waliojenga Zahanati hiyo.
Masista Waabuduo Damu ya Kristo wakifurahia taswira za picha za mnato kutoka kwenye kamera.
Jenereta la Zahanati ya Da.Ma Africa linalotumika kutoa umeme katika Zahanati hiyo.
Muonekano wa nje wa jengo la Zahanati ya Da.Ma Africa kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Wanakijiji wa Vikawe na wageni waalikwa wakiingia kukagua Zahanati hiyo mara baada ya kuzinduliwa.
No comments:
Post a Comment