Na Philemon Solomon wa Fullshangwe Dar es salaam
WAKAZI wa Kibasila Kata ya Gerezani ambao nyumba zao zilibomolewa
kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo kasi wamepinga fidia
inayotolewa na DART wakidai inapingana na sheria.
Akizungumza katika mkutano na wananchi hao Dar es Salaam juzi,
Wakili Dk. Edmund Mvungi kutoka Shirika la Wanasheria wa South Law
Chambers alisema malipo hayo ni batili.
Alisema DART kwa siku kadhaa mfululizo imekuwa ikitoa matangazo
kwenye vyombo vya habari kuwa waliobomolewa waende kuchukua fedha za
fidia.
Alisema DART walidai kuwa wakazi hao waliobomolewa nyumba hizo
watalipwa donge nono la fidia ya sh.milioni 30 kufidia ardhi yao
iliyotwaliwa na serikali.
Alisema sheria haielekezi hivyo fidia ya ardhi hutolewa baada ya
bomoabomoa kwani fidia ni matokeo ya makubaliano kati ya serikali na
wamiliki halali wa ardhi inayochukuliwa na kuwa sheria inaagiza kuwa
kigezo ni bei ya soko.
Amesema DART kwa makusudi wameamua kukiuka sheria kwa kuanza
kutangaza kufanyika kwa malipo hayo licha ya jambo hilo kuwa mahakamani.
Alisema fidia hiyo ni kinyume na sheria hivyo wao wamependekeza
kila mmoja wao kulipwa sh. bilioni 2 kama fidia ardhi yao na usumbufu wa
kubomolewa makazi yao.
Alidai wanakusudia kufungua kesi mahakamani dhidi ya Mkurugenzi wa
DART Kosmas Tekule kwa kukikuka sheria kwa kuanza kuwarubuni baadhi ya
wananchi hao na kuanza kulipa fidia wakati suala hilo lipo mahakamani.
Katika hatua nyingine alisema wanakibasila hao hawawatambui wenzao
28 ambao wamerubuniwa kuchua fidia hiyo na kupitia kamati yao bandia
ambapo walidai uongozi wanaoutambua ni ule unaosimamia kesi yao namba
44.
Viongozi hao wanaotambulika wametajwa kuwa ni Abdalla Mkongo, Jumbe Lilla, Hussein Batenga na Athman Kiwaga.
Alisema matangazo yanayotolewa na DART ni uchochezi na uvunjaji wa
sheria kwani anayetoa matangazo hayo anaingilia kesi iliyopo mahakamani.
No comments:
Post a Comment