Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, May 25, 2010

Jumuiya ya Afrika mashariki kupeleka kilio kwa wamachinga

Jumuiya ya Afrika mashariki kupeleka kilio kwa wamachinga

Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya


WAFANYABIASHARA wadogo, maarufu kwa jina la wamachinga hawana nafasi ya kunufaika na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, imefahamika.

Akizungumza jana na Viongozi wa taasisi mbalimbali mkoani Mbeya, Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Aboud Mohamed Aboud, alisema katika Itifaki ya soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni marufuku kwa wamachinga kutoka nchi moja kwenda kufanya biashara katika nchi nyingine ndani ya Jumuiya hiyo.

Alisema wafanyabiashara wanaoruhusiwa kutoka nchi moja kwenda nyingine ni wale wenye mitaji mikubwa, ambao uwekezaji wao unaweza kuleta tija katika maeneo wanakokwenda kufanya biashara hizo.

"Tunahitaji wafanyabiashara wakubwa, wenye uwezo wa kufanya uwekezaji wenye tija, lakini sio wamachinga, hizi biashara ndogo ndogo zitabaki kuwa fursa kwa wananchi wa maeneo ya nchi husika tu," alisema Aboud.

Alitoa mfano kuwa ikiwa mtu anatoka nchi nyingine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na anahitaji kufungua hoteli katika nchini, lazima hoteli yenyewe ianzie hadhi ya nyota tatu kwa Tanzania Bara na hadhi ya nyota nne kwa Tanzania visiwani.

"Haturuhusu mtu aje kujenga banda la kuwa guest house (nyumba ya kulala wageni), tunahitaji awe muwekezaji wa kweli kwa maana ya kuwa na mtaji mkubwa ili wananchi wetu waweze kunufaika na uwekezaji ake," alisema Aboud.

Hata Mwenyekiti wa Mkoa wa chama cha PPT Maendeleo, Godfrey Devis alimuuliza Aboud kuwa ikiwa wamachinga wa Afrika Mashariki hawaruhusiwi kwenda nchi nyingine ndani ya jumuiya, inakuwaje hivi sasa nchini kuna wamachinga tele kutoka nchini China.

Akijibu swali hilo, Aboud alisema hakun uhalali wa watu kutoka nje ya nchi kuja kuwa wachuuzi nchini, na kuwa kama wapo ni wahalifu kama walivyo wahalifu wengine na kuwa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Wamachinga wawe wa kutoka China au Rwanda, wote ni wahalifu, wachukuliwe hatua na wala tusihukumu nchi kwa udhaifu wa mtendaji mmoja wa Serikali," alisema Aboud.

Aidha Naibu Waziri huyo alisema wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamefunguliwa milango ya kuajiriwa katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya, endapo tu watafuata taratibu za uhamiaji katika nchi husika.

Hata hivyo alisema kuwa ajira hizo ni kwenye sekta binafsi pekee na kamwe hazihusiani na nafasi zitakazokuwa zikitolewa kwenye sekta ya umma.

Waziri Aboud alisisitiza kuwa suala la ukazi wa kudumu kwa wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki halipo katika itifaki wala mkataba wa Jumuya hiyo.
"Suala la ukazi wa kudumu halipo kwenye mkataba, isipokuwa litasimamiwa na sheria za nchi huzika," alisema Aboud.

Kuhusu soko la pamja, Naibu Waziri huyo alisema Tanzania imeanza kunufaika ambapo imeuza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 353 katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa pia Tanzania iliagiza bidhaa kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zenye thamani ya dola za Marekani milioni 202,ambao katika suala la uwekezaji umeongezeka kutoka miradi 505 iliyowekezwa mwaka 2005 na kufikia miradi 871 ikiwa na thamani ya Dola milioni 66.8.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...