Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, May 26, 2010

MICHUANO YA 9 YA MPIRA WA KIKAPU ILIVYOFANA



Amina Athumani

MICHUANO ya 9 ya Mpira wa Kikapu ya Klabu Bingwa Tanzania (NBL) imemalizika hivi karibuni huku ikiacha maswali mengi na changamoto kedekede kwa uongozi wa Shirikikisho la mchezo huo (TBF) ambao ndio wenye dhamana ya kusimamia mchezo huo.

Changamoto na maswali mengi yaliyopatikana katika mashindano hayo ni ile hali ya mikoa mingi kushindwa kushiriki mashindano hayo huku maswali yakibaki kwenye tatizo la kukwamisha timu hizo huku viongozi hao wakiamini suala zima la wadhamini ndio kikwazo kikubwa.

Michuano hii ambayo ilifanyika katika uwanja wa ndani wa Taifa Dar es Salaam iliitawaza timu ya Savio kuwa bingwa mpya wa NBL baada ya kuivua ubingwa timu ya JKT katika fainali iliyokuwa kali na yakusisimua.

Kwa pande wa wanawake Jeshi Stars ilikuwa bingwa baada ya kushinda michezo yote nane iliyocheza huku mchezo wa mwisho ikiifunga Polisi Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo timu ya Savio, JKT, Jeshi Stars na Polisi Dar es Salaam zitaiwakilisha nchi katika mashindano ya kanda ya tano yatakayofanyika nchini Burundi mwezi Agost mwaka huu.

Mashindano haya yalikuwa na mbwembwe nyingi kwa upande wa timu shiriki na hata kuleta upinzani na uadui baina ya klabu kwa klabu ama wachezaji kwa wachezaji.

Uwadui huu unaweza kuwa ule uliotokea katika hatua ya fainali iliyozikutanisha timu za jijini Dar es Salaam huku JKT ambao ni Mabingwa watetezi wa NBL wakichuana ya na timu ya Savio ambao nao ni mabingwa wa Ligi mpira wa kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA).

Chuki na hasira zilitawala katika mchezo huo ingawa kwa namna moja ama nyingine zilidhibitiwa hasa pale mchezaji wa timu ya JKT, Francis Mlewa kumtwanga mchezaji wa Savio Jije Makani teke katikati ya mchezo na mara baada ya mchezo kumfuata tena na kumpiga ngumi ya mdomoni hali iliyomsababishia mchezaji huyo maumivu.

Katika hali ya kawaida tu ya kibinaadamu hali hiyo inaweza ikawa uwadui wa muda mrefu baina ya wachezaji hao ama klabu zao kutokana na kwamba tayari klabu ya Savio imeripoti katika kituo cha polisi juu ya shambulio hilo.

Bado haijafahamika kuwa chanzo ni nini hasa lakini kimichezo tunaweza kusema ni utovu wa nidhamu uliosababisha wachezaji wa upande mmoja kuwa na hasira zilizopelekea kuumizana kiasi hata cha kamati ya mashindano kuliingilia kati suala hilo ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu kali kwa wachezaji waliofanya utovu wa nidhamu.

Kitendo hicho kiliwakera sana viongozi wa TBF hasa ikizingatiwa kuwa mchezaji huyo aliyafanya mambo hayo mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Taifa (BMT) Kanal mstaafu Iddi Kipingu.

Kitendo hicho cha utovu wa nidhami kimepelekea kuharibu hata sifa ya mashindano ama michezo ambapo Katibu Msaidizi wa TBF , Michael Malue analizungumzia suala hilo na kusema kuwa wametoa adhabu ya kumfungia mchezaji huo kwa kutojihusisha na mchezo huo ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

"Adhabu hii imeanza April 17 mwaka huu hadi April 16 2011 baada ya TBF Kukaa kikao na kupitia kanuni za mashindano na kutoa adhabu hiyo kuhusu makosa ya nidhamu ya mchezo kwa kutumia kifungu cha 7.0 kipengele 7.1 kinacho ainisha aina ya adhabu,"anasema Maluwe.

Maluwe anasema mbali na suala hilo la utovu wa nidhami kujitokeza katika mashindano hayo ya NBL pia wamekabiliana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya mfumo mzima wa mashindano hayo na kwamba wanaweka kama ajenda katika kikao cha kamati ya utendaji ya TBF kitakachofanyika baadae.

Anasema changamoto zenyewe zitakuwa ni pamoja na kutokuwa na viwanja vya uhakika kwa mashindano ya Taifa hasa katika hali ya nvua na jua na kwamba hali ya nvua imefikia hata kufanya mashindano hayo yasimame kwa muda kutokana na uwanja wanaoutumia kwa sasa kuendeshea mashindano mbalimbali kuwa katika hali mbaya ya kuvuja mara mvua inaponyesha ikiwa ni pamoja na vifaa vya uendeshaji wa mashindano.

Anasema tatizo kubwa na mapungufu yaliyoonekana katika mashindano hayo ni kutokuwa na mawasiliano baina ya TBF na wanachama wake ambao ni mikoa na kwamba timu za mikoani hazina maandalizi ya kutosha na kwamba kutokuwa na wadhamini ni mapungufu makubwa yaliyofanya ushiriki kutoka mikoani kuwa ni mdogo katika michuano hiyo ya NBL.


Maluwe anasema kutokana na hayo yote yaliyojitokeza katika mashindano ya mwaka huu watajipanga katika NBL 10 katika kuboresha hatua zote stahili za kiufundi na kiutawala na kwamba wanategemea mara baada ya kukutana katika kikao cha kamati ya utendaji kupendekeza mambo mengi yahusuyo mchezo huo.

Anasema kwa upande wa ufundi wanahitaji kuwa na vifaa vya kisasa vya kuendeshea michezo 'Twety four Sec (24sec), stop watch ambayo itamuwezesha kila mmoja aliyekuwepo uwanjani kuweza kuona muda na kuondoa malalamiko ya kuibiwa muda au kuongezewa muda na kiutawala kuboresha mawasiliano na viongozi wa mikoani na klabu ili ushiriki wao uwe mkubwa

Maluwe anasema kuna ulazima wa kuweka kanuni za mashindano kwa nia ya kukuza mchezo huo hasa katika usajili wa wachezaji ili kutoa nafasi kwa wachezaji wa mikoani kucheza na kukuza vipaji vyao kuliko kukwepa harama za kupeleka timu kwenye kituo na kutaka kuwatumia wachezaji kutoka mikoa mingine.

Maluwe hakusita kuielezea ligi ya NBL ya mwaka huu na kusema ligi hiyo ilikuwa ni nzuri pamoja na mapungufu madogo yaliyopo wamefanikiwa kufanya mashindano kwa mujibu wa kalenda ya TBF na kwamba wanapongeza ushirikiano uliokuwepo kwenye mashindano hayo kuanzia waamuzi, viongozi wa klabu za mikoani za jijini Dar es Salaam na wachezaji pamoja na wapenzi na mashabiki waliofika viwanjani hapo.


Anasema TBF imebaini mapungufu yaliyojitokeza katika kanuni za kusajili wachezaji ambapo mikoa iliyoshiriki ligi ya NBL wamesajili wachezaji wanaocheza ligi za Dar es Salaam na kwamba katika mashindano ya 10 ya NBL, TBF itahakikisha kanuni za mashindano hayo zinawapa nafasi kwachezaji wa mikoani kuchezea mikoa yao na kwamba klabu za mikoani zisitegemee wachezaji wanaocheza ligi za Dar es Salaam.

Anasema pia suala hilo liwe changamoto kwa makocha wote wa Tanzania kwa wale waliopata nafasi ya kwenda nchini Marekani kwenye ziara ya michezo ya mafunzo watoe mafunzo hayo kwa wachezaji wapya na chipkizi.

Maluwe alipongeza klabu ya Dodoma Spurs na Kilimanjaro Baptisti kwa kuleta wachezaji halisi kutoka katika mikoa yao na kwamba wachezaji hao wameonesha wanaweza kufanya vizuri isipokuwa kinachowakwamisha ni ukosefu wa mashindano mengi ya ushindani na kuwapongeza makocha wa timu hizo Yasini Musira wa Dodoma na William Mukunya kwa kuwaleta vijana wengi ambao wameweza kuzisumbua timu kongwe. .

Mikoa mingine imetakiwa kuiga mfano wa timu hizo kwa kutumia wachezaji halisi wa mikoa yao ili kuweze kuwa na tofauti katika mashindano yajayo na hata yale ya Taifa 'Taifa Cup' yatakayofanyika mwezi Julai mwaka huu.


TBF imelipongeza jeshi la polisi la Changombe kwa kutoa sapoti ya ulinzi katika mashindano hayo hasa katika kipindi cha mwanzo cha mashindano hayo na kwamba katika kipindi cha mwisho Jeshi hilo halikujitokeza hali iliyopelekea kutoa mwanya wa matukio kama ya wachezaji kupigana na kuumizana.

Maluwe anasema TBF imeshachukua hatua kali za kinidhamu na kwamba klabu ya Savio imetoa ripoti katika kituo cha polisi juu ya shambulio hilo.

Kwa ujumla mashindano ya NBL yalileta msisimko katika ushindani wa kimichezo na kwa mapungufu yaliyojitokeza ni ya kurekebishika cha msingi kuboresha nidhamu kwa kila mchezaji ili dhana ya michezo kuwa ni amani na urafiki idumike na wachezaji waliokoseana katika mashindano hayo wasameheane.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...