Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, June 4, 2011

MBOWE MASHAKAN TENA MAHAKAMANI...??



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imeagiza tena Jeshi la Polisi kumkamata Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Bw. Freeman Mbowe baada ya kushindwa kujisalimisha mahakamani katika kesi inayomkabili.
Akitoa hukumu dhidi ya washtakiwa wengine waliojisalimisha mahakamani baada ya kushindwa kuhudhuria katika mahakamani hapo Mei 27 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Bw. Charles Magesa alisema kitendo cha mshitakiwa wa kwanza katika shauri hilo kushindwa kujisalimisha labda anataka kukamatwa na polisi.
Mahakama hiyo awali, iliamuru Mwenyekiti huyo pamoja na viongozi wengine akiwemo Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Willibrod Slaa, wabunge wawili wa chama hicho, Bw. Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini) na Bw. Godbless Lema (Arusha Mjini) wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo baada ya kushindwa kuhudhuria katika kesi inayowakabili ya kufanya kusanyiko lisilo halali Januari 5 mwaka huu.
Washtakiwa wengine ambao mahakama ilitoa hati ya kukamatwa ambao hata hivyo walijisalimisha mahakamani siku mbili baadaye ni pamoja na mchumba wa Dkt. Slaa, Bi. Josephine
Mushumbusi, Bw. Richard Mtui, Bi. Aquiline Chuwa na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Bw. Samson Mwigamba.
Pamoja na washtakiwa na wadhamini wao kutofika mahakamani, hata Mawakili wao, Bw. Method Kimomogolo na Bw. Albert Msando pia hawakuwepo mahakamani wakati hati hiyo inatolewa, lakini
washtakiwa Bw. Joseph Selasini (Mbunge wa Rombo) na Bw. Dadi Igogo pia hawakuwepo mahakamani siku hiyo, na mahakama haikutoa hati ya kuwakamatwe kwa sababu wadhamini wao walikuwapo.
Washtakiwa waliohudhuria mahakamani hapo siku hiyo ni pamoja na Bw. Nai Steven, Bw. Mathias Valerian, Bw. John Materu, Bw. Daniel Titus, Bw. Juma Samuel, Bw. Walter Mushi, Bw. Peter Marua na Bw. Erick Makona.
Hakumu Magesa alisema mshitakiwa wa kwanza (Mbowe) baada ya kutolewa hati ya kumkamata au kujisalimisha mahakamani hakufanya hivyo hadi jana wala mdhamini wake, hivyo Ofisa Inchaji wa Polisi anatakiwa kumkamata kwani ni wajibu wake kutekeleza amri halali ya mahakama ni si vinginevyo.
“Wote walipewa masharti ya kufika mahakamani kama ulivyo utaratibu na iwapo wanapatikana na udhuru wa kibinadamu basi ni wajibu wa wadhamini wao kuhakikisha wanafika mahakamani kueleza kilichowasibu. Kimsingi si sahihi kutofika mahakamani bila taarifa, hivyo Ofisa Inchaji amkamate na kufikishwa mahakamani,” alisema.
Bw. Ndesamburu alinusurika kwenye hukumu hiyo baada ya Mdhamini wake, Bw. Reuben Ngowi kuibuka mahakamani hapo na kutoa udhuru uliomkuta mshtakiwa huyo pamoja na yeye mwenyewe, ambapo Hakimu Magesa alikubaliana naye na kufuta amri hiyo, hivyo kuachiwa huru.
Katika hukumu dhidi ya washitakiwa wengine waliojisalimisha pamoja na wadhamini wao, walipewa onyo kali na kutakiwa kutorudia kosa hilo kwani kufanya hivyo ni kukiuka maagizo halali ya mahakama.
Alisema amepitia hoja za wakili wa upande wa utetezi, na kwa kuzingatia sababu zilizotolewa mahakamani, aliamua kufuta amri hiyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...