Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, April 5, 2012

NI UHONDO JUU YA UHONDO TAMASHA LA PASAKA


Mary Mwanjelwa
BALOZI wa Tanzania nchini China, Philip Marmo, ni miongoni mwa wageni waalikwa watakaohudhuria tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mratibu wa tamasha hilo, Alex Msama wa Kampuni ya Msama Promotions, alisema Dar es Salaam jana kuwa Marmo amethibitisha kuhudhuria ili kutoa mchango wake kwa yatima.
Alisema Marmo ambaye kabla ya kuwa Balozi aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, ameahidi ataambatana na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Mary Mwanjelwa (CCM) kuhudhuria tamasha hilo la Jumapili.
Msama alisema Marmo aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbulu, alidai ameshawishika kuhudhuria tamasha hilo kutokana na kushirikisha waimbaji kutoka sehemu mbalimbali Afrika.
Alisema Marmo amelisifia tamasha la Pasaka kwa kusema kwamba ni jambo jema zaidi kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane, akiunga mkono kauli ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Athuman Mfutakamba.
Mfutakamba ambaye pia ni Mbunge wa Igalula, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, alikaririwa hivi karibuni akisema amefarijika na mwamko wa Msama Promotions kwa kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watoto yatima na wanawake wajane.
Tamasha la Pasaka linatarajiwa kufanyika Jumapili, Sikukuu ya Pasaka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Jumatatu ya Pasaka Aprili 9 mwaka huu, lengo kubwa ni kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mtaji wa biashara wajane.
Tamasha la mwaka huu litapambwa na waimbaji nguli wa muziki wa Injili wakiwamo Rebecca Malope wa Afrika Kusini, Rose Muhando, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti Faraja Ntaboba, Ephraim Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival.
Mgeni rasmi Uwanja wa Taifa anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na pia kwenye Uwanja wa Jamhuri, mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika, Job Ndugai.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...