TOVUTI ya
Kandanda.galacha.com ya jijini Dar es Salaam imejitosa kudhamini Tuzo za
Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 upande wa soka.
Wakizungumza kwenye
mkutano na waandishiwa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa tovuti
hiyo, ambayo pia ina tovuti nyingine iitwayo kandanda.co.tz, Erick Zomboko
alisema tovuti yao inahusiana na masuala ya mpira wa miguu na wameona wajiunge
katika hatua ya kuendeleza michezo hapa nchini.
Alisema wanathamini
tuzo hizo zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA),
hivyo pamoja na upya wao katika masuala ya tasni ya habari wameona waunganishe
nguvu kusaidiana na TASWA.
Alisema katika udhamini
wao watatoa tuzo maalum kwa washindi upande wa mpira wa miguu na pia watatoa
fedha taslimu kwa washindi hao, lakini hawawezi kutangaza kiasi cha fedha
watakachowapa washindi hadi siku hiyo.
Zomboko alitaja
watakaowania tuzo hiyo kuwa ni wale waliotangazwa na Kamati ya Tuzo upande wa
mpira wa miguu kwa wanaume, ambao ni Juma Kaseja (Simba), Aggrey Morris na John
Bocco wote wa Azam, wakati mpira wa miguu wanawake ni Fatuma Mustapha (Sayari),
Ito Mlenzi (JKT), Mwanahamisi Omary
‘Gaucho’ na Asha Rashid ‘Mwalala’ wote wa timu ya Mburahati Queens.
Wachezaji wengine
ambao watawania tuzo hiyo ni wale wa nje wanaocheza soka Tanzania, ambao ni
Haruna Niyonzima (Yanga), Emmanuel Okwi (Simba) na Kipre Tchetche (Azam).
“Haya ni makundi
matatu tofauti, ambayo yametangazwa na Kamati ya Tuzo ya TASWA, tutakachofanya
sisi mshindi wa kila kundi tutampa zawadi yake siku hiyo ya sherehe, itakuwa ni
tuzo pamoja na kiasi fulani cha fedha, tuzo ambayo itakuwa na jina la mhusika,”
alisema na kuongeza kuwa udhamini huo ni kiasi cha sh. Milioni sita.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa TASWA inayoandaa tuzo hizo, Maulid kitenge aliishukuru tovuti
hiyo na kusema licha ya kwamba wana udhamini wa Kampuni ya Bia ya Serengeti,
lakini bado hautoshi, hivyo wadau mbalimbali wanakaribishwa kuwaunga mkono
katika juhudi zao za kuwatuza wanamichezo.
Sherehe za
kuwazawadia Wanamichezo Bora wa Tanzania zinatarajiwa kufanyika Alhamisi wiki
hii ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, ambapo michezo mbalimbali
itazawadiwa.
Wakati huohuo,
Kitenge alisema Jumatatu saa tano asubuhi TASWA wanataraji kufanya mkutano na
waandishi wa habari, ambao pamoja na mambo mengine watatangaza mgeni rasmi wa
sherehe hizo pamoja na burudani mbalimbali kwenye mgahawa wa City Sports
Lounge.
No comments:
Post a Comment