Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, August 28, 2010

DKT WILLIBROD SLAA AZINDUA KAMPENI LEO


Mwenyeki wa chama cha CHADEMA,Freeman Mbowe akimkabidhi vitabu vya Ilani ya chama hicho kwa mgombea Urais wa chama hicho Mh Willbrod Slaa leo jioni katika viwanja vya Jangwani jijini Dar mara baada ya kuizindua.


Wanachi waliojitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni na Ilani ya chama cha CHADEMA leo jioni katika viwanja vya Jangwani jijini Dar

Wasanii wa Bongofleva Dani Msimamo pamoja na Mkoloni wakiimba jukwaani.
Na Waandishi Wetu

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa ameeleza vipaumbele vyake katika muda mfupi, kati na mrefu akianza na mambo makuu matatu endapo atashinda nafasi hiyo.

Dkt. Slaa alieleza hayo Dar es Salaam jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili juu ya mipango yake na jinsi atakavyoitekeleza, endapo atapata ridhaa ya Watanzania kuwa kuongoza serikali ya awamu ya tano.

Mambo hayo ni mabadiliko ya katiba, kurejesha taifa katika misingi ya maadili na uzalendo iliyopotea na uwajibikaji serikalini, ambayo yatatekelezwa ndani ya siku 100.

"Tutakapozindua kampeni zetu tarehe 28 tutazindua na ilani yetu pamoja na action plan (mpango wa utekelezaji). Huu ni uchaguzi utakaotupeleka kwenye mabadiliko makubwa," alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Slaa mpango huo utaonesha jinsi ya kufanya mabadiliko hayo, ili kulirejesha Taifa katika mstari kutokana na kupoteza uadilifu na kuendesha nchi kwa misingi ya kubaguana.

Alitolea mfano wimbo maarufu wa CCM uanaohubiri 'kuwaleta wapinzani, kuchanachana na kuwatupa' kuwa unaimbwa hata mbele ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho lakini hawasemi lolote wakati unahubiri dhana ya mauaji.

Akizungumzia utendaji wa serikali, mgombea huyo alisema kwa sasa serikalini hakuna uwajibikaji wala maamuzi na kero za wananchi zinatatuliwa kisiasa.

Dkt. Slaa alitumia muda mrefu kuzungumzia mabadiliko ya katiba, huku akiainisha vipengele vyenye matatizo kwenye katiba ya sasa, hasa madaraka makubwa aliyopewa rais, yanayompa nafasi ya kuteua watu wengi, ingawa si rahisi kwake kuwafahamu wote.

Alisema atakapoingia ikulu ataunda serikali ndogo yenye ufanisi ya mawaziri wasiozidi 20 ili kupunguza matumizi ya serikali yasiyokuwa ya lazima.

Kwa mujibu wa mgombea huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Serikali ya sasa yenye mawaziri 47 ni mzigo kwa walipa kodi, katika mishahara, marupurupu, magari na huduma nyingine.

Alitoa mfano wa Uingereza yenye watu zaidi ya milioni 70, ina mawaziri wasiozidi 20.

Akizungumzia baadhi ya gharama zinazoendesha serikali, alitoa mfano wa magari (mashangingi) ambayo yanauzwa sh. milioni 200 kila moja, akisema kila waziri anatembea na zahanati nne zinazogharimu sh. milioni 50 kila moja.

"Hiyo anasa hatuiwezi, lazima tuachana nazo...Mtu asitarajie akienda serikali ya CHADEMA anakwenda kula. Hili tutaanza nalo kwa katiba ya sasa na baadaye kuliingiza katika katiba tutakayounda, ili idadi ya mawaziri wanaotakiwa ijulikane, asijekutokea rais mwingine akaweka anaowataka kwa kuzingatia uswaiba," alisisitiza.

Mgombea huyo alitoa mfano wa Wilaya ya Karatu ambako chama chake kilikuwa kinaongoza serikali na CCM kuwa wapinzani, kuwa waliweka watendaji ndani ya miezi mitatu walifungwa karibu wote kwa ulaji.

Mambo mengine ambayo Dkt. Slaa anatarajia kuweka mfumo wa utawala utakaopunguza matumizi na kuongeza uwajibuikaji, kama kuondoa nafasi za wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa na kazi zao kurejeshwa kwa wakurugenzi wa Halmashauri na baadaye katika majimbo, kuongeza uwajibikaji kwa mawaziri kuthibitishwa na bunge, mawaziri kutokuwa wabunge na rais kushinda kwa zaidi ya nusu ya kura.

Pia CHADEMA kinakusudia kuruhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, kuweka mipaka ya kiutendaji katika mihimili mitatu ya serikali, bunge na mahakama, kuainisha shughuli za usalama wa taifa na kuunda tume huru ya uchaguzi.

Vile vile Dkt. Slaa alisema wanakusudia kuondoa dhana potofu kuwa kila kitu kuhusu jeshi ni siri, bali lijulikane kuwa ni huduma ya umma, bali siri ni mbinu, mikakati na vyombo vyake, lakini si masuala kama ya kashfa ya Meremeta, iliyofishwa kwa sababu ya kuhusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Alisema pia wanakusudia kuwa na jeshi dogo lenye vifaa vya kisasa na lenye ufanisi. Pia watafufua kikosi cha nyumbu ili jeshi litumike kutengeneza magari na vifaa vingine.

Akidokeza juu ya kampeni yake, alisema asingeweza kuweka wazi mikakati, lakini wanayo mambo mengi ya kuzungumza, zikiwamo nyaraka mbalimbali za ufisadi na jinsi serikali inavyotumia fedha za walipakodi kuisaidia CCM.

"Uchafu ndani ya serikali uko kila sehemu, tunazo documents (nyaraka), kwenye serikali za mitaa huko ndo usiseme ufisadi wao ninaujua kila sehemu. Kwa ufupi serikali nzima imeoza na haina uwezo wa kujisafisha," alisema.

Kuhusu ajira, Dkr. Slaa alisema serikali yake itahakikisha kila bajeti inayopangwa inalenga kuongeza kiwango fulani cha ajira badala ya kusubiri wawekezaji ndio walete ajira.

Katika kipango ya muda wa kati ndani ya miaka mitatu, Dkt. Slaa alisema kilimo cha zalishaji wa chakula ama kwa kutumia uwezo wa serikali au kwa kutangaza tenda za kimataifa ili kuondoa aibu ya kila mwaka ya kuomba chakula kwa wahisani.

"Mfano yale mabilioni ya JK yalifanya nini, Kina Kapuya (Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Juma) wanatoa takwimu kuwa watu 44,000 wamenufaika. Watu 44 elfu ni kitu gani kati ya milioni 40? fedha kama hizo zingeweza kutumika kuinua kilimo cha umwagiliaji na taifa likajitegemea kwa chakula," alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuziponda trekta ndogo (powertiller) kuwa zimenunuliwa bila utafiti katika baadhi ya maeneo, na matokeo yake zimeshindwa kulima kwa kuwa zinatumia nguvu ya binadamu.

Vile vile Dkt. Slaa alisema ni mipango yake mingine miji na kuweka miundombinu ya umma itakayopunguza msongamano wa magari mijini.

Alisema kwa sasa ujenzi unaondelea ni wa majumba makubwa lakini hakuna miundombinu ambayo muda wake muafaka ni sasa, kwa huko baadaye itakuwa si rahisi kulipa fidia.

Kwa upande wa elimu alisema serikali lazima igharamie masomo hadi kidato cha sita badala ya kufuta tu mchango wa UPE ikasema kuwa imegharamia elimu.

Akizungumzia maisha binafsi, Dkt. Slaa alikiri kuwa aliwahi kuwa padri na vyeo alivyowahi kushika ndani ya kanisa Katoliki, kama Makamu wa Askofu, Mkurugenzi wa Maendeleo na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu.

Alitumia nafasi hiyo kumtambulisha mke wa sasa, Josephine, na kuweka bayana kuwa kuanzia mwaka jana alitengana na Rose Kamili ambaye katika maisha yao, bila kufunga ndoa kikanisa, walipata watoto wawili

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...