Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, September 29, 2010

Deo: Nitatimiza ndoto na kuleta matumaini



VYAMA mbalimbali vya siasa nchini na wagombea wa nafasi za uongozi kwa tiketi ya vyama hivyo, wapo katika kampeni ya kunadi sera na ilani ya vyama vyao kwa wiki ya sita sasa.

Wapiga kura katika maeneo mengi, wamekuwa wakilishwa ahadi za matumaini ya maendeleo na wagombea ili jamii kubwa iweze kuondokana na umaskini walionao.

Lengo la wagombea wengi ni kuhakikisha majimbo yao yanakuwa mfano wa kuigwa dhidi ya mengine. Kazi kubwa inayofanywa na wagombea kwa sasa ni kuwashawishi wapiga kura wachague viongozi bora wenye dhamira ya kuharakisha maendeleo.

Bw. Mushi Deo (40) ni mgombea udiwani Kata ya Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye anasema, dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo ni kutimiza ndoto ya matumaini kwa wananchi wa kata hiyo ili kuwa ya mfano.

Katika mahojiano na Majira, Bw. Deo anasema kata hiyo inahitaji kiongozi makini anayeweza kumaliza kero za wananchi zilizodumu muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Mwaka 2005 niliwania ubunge wa jimbo lakini kura zangu hazikutosha, mwaka huu nimeamua kushuka ngazi ya chini kwa sababu wananchi wanahitaji mchango wangu ili waweze kutimiza ndoto yao ya kuwa na maisha bora,” alisema.

Anasema jambo ambalo limemsukuma kuwania nafasi hiyo ni kuonesha uwezo wake katika kuwatumikia wananchi kama kijana, kutatua kero zao kwa wakati na kuondoa umaskini uliopo kwa jamii kubwa akitumia elimu aliyonayo, maarifa pamoja na ubunifu kuboresha maisha yao.

Bw. Deo ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Sayansi na Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema pamoja na kata hiyo kukabiliwa na matatizo lukuki, zipo kero sita ambazo atazipa kipaumbele cha kwanza ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Anasema kero hizo zimetokana na uongozi mbaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo wananchi kukosa huduma muhimu kama maji, barabara, elimu na afya.

Hali hiyo imechangia vijana wengi kujihusisha na vitendo vya uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu ya kukosa ajira za uhakika.

“Kama wananchi watanipa ridhaa ya kuwa diwani wao, nitahakikisha ilani ya chama changu inatekelezwa kwa vitendo ambapo katika sekta ya afya, nitajenga zahanati ya kata ndani ya miaka miwili na kutoa matibabu bure.

“Zahanati hii, itakuwa ikilaza wagonjwa wa kawaida, wanawake wajawazito, watoto, wazee pamoja na kuajiri wataalamu waliobobea katika fani ya huduma za afya,” anasema Bw. Deo na kuongeza kuwa, atahakikisha mapato katika kata yanasimamiwa vizuri ili kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi.

Anaongeza kuwa, tatizo la ukosefu wa zahanati ya kata limekuwa likichangia wanawake wengi kufuata huduma Hospitali ya Mwanyamala ambayo haitoi huduma za afya kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya mgonjwa.

Akizungumzia sekta ya maji, Bw. Deo anasema inashangaza kata hiyo kukabiliwa na tatizo sugu la maji safi na salama wakati Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), ina ofisi katika kata hiyo.

Anasema asilimia kubwa ya Watanzania hawapati maji safi na salama lakini pamoja na kilio hicho, watawala ambao wametangulia hawakulipa kipaumbele suala hilo badala yake, wamelipa kisogo na kuwaacha wananchi wakiteseka kwa kukosa huduma hiyo muhimu.

“Ni jambo lisilowezekana kwa DAWASCO, kuwa na ofisi katika kata yetu lakini wakazi wa kata hii wasinufaike na huduma wanazotoa, hakika inashangaza,” anasema.

Anaongeza kuwa, kama atapata ridhaa ya kuwa diwani wa kata hiyo, atahakikisha katika kipindi cha miaka mitano, kila mwananchi atakunywa maji safi na salama.

Anasema kero nyingine inayowakabili wananchi ni barabara. Kero hiyo ni kilio cha muda mrefu lakini bado imefumbiwa macho na viongozi waliotangulia wakati maeneo wanayoishi viongozi wa Serikali zimewekwa miundombinu mizuri ya kuvutia.

Bw. Deo anasema, ujenzi wa miundombinu ya barabara haupaswi kubagua maeneo kwani kila mwananchi anawajibika kulipa kodi hivyo ameahidi kusimamia ujenzi wa barabara katika kata hiyo ili wananchi wake waweze kunufaika na ujenzi huo.

"Ndani ya Manispaa kuna fungu linalotolewa kwa ajili ya matengenezo ya barabara, fungu hili litakuwa halitumiki ipasavyo ndio sababu inayochangia barabara hizi kutofanyiwa ukarabati unaostahili,” anasema.

Anasema fedha za ujenzi huo hazitatoka mfukoni kwake bali kwa kushirikiana na viongozi ambao watakuwepo madarakani pamoja na marafiki zake wa ndani na nje ya nchi, atahakikisha wanatafuta wafadhili ambao watatoa fedha ili kufanikisha ujenzi huo.

Mbali na wafadhili hao, ilani ya chama hicho pia itafanikisha ujenzi huo kwani dhamira ya viongozi wa juu wa chama hicho Dkt. Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wake Bw. Freeman Mbowe, ni kuhakikisha sekta mbalimbali, zinapiga hatua kubwa ya maendeleo.

Akizungumzia suala la elimu, Bw. Deo anasema kwa muda mrefu sasa, kata hiyo inakabiliwa na tatizo la vijana na watoto kukosa elimu kutokana na upungufu wa shule.

Mkakati wake ni kuhakikisha kila mtoto ndani ya kata hiyo, anapata elimu bora ambayo itatolewa bure kuanzia shule ya awali, sekondari hadi vyuo vikuu.

Ili suala hilo liweze kufanikiwa, atashirikiana na Serikali iliyopo madarakani na wadau wa elimu kuhakikisha zinajengwa shule kuanzia chekechea hadi sekondari.

“Siwezi kuwashau yatima na waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI, nitahakikisha wanapata fursa ya kusoma na kusaidiwa ili waweze kujipatia kipato cha uhakika, kukuza mitaji yao na kujikomboa kiuchumi,” anasema Bw. Deo na kuongeza kuwa, kupitia utaratibu huo, yatima wote watapata elimu bure na waliopo sekondari watatafutiwa wafadhili.


Anasema mpango huo utakuwa umekamilika ndani ya mwaka mmoja ili kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Anaongeza kuwa, Manispaa imekuwa na kawaida ya kutenga fedha hivyo kinachohitajika ni ufuatiliaji ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Bw. Deo anasema, lipo tatizo la waathirika wa dawa za kulevya katika kata hiyo kutokana na Serikali kutowajengea vijana mazingira mazuri ya kuwanusuru na janga hilo.

Vituo vingi vya polisi vimekuwa vijiwe kwa kurundika vijana badala ya kutafutiwa njia mbadala ambazo zitawafanya waachane na matumizi ya dawa hizo. Kama atakuwa diwani wa kata hiyo, atashirikiana na watendaji wa kituo cha kudhibiti dawa za kulevya ili kuwasaidia vijana hao waachane na matumizi ya dawa hizo.

“Ili niweze kufanikisha lengo hili, nitaunda Serikali ya Kata ambayo itakuwa ikishirikiana na Mwenyekiti wa Mtaa ili kutafuta mbinu mbadala za kuwaletea wananchi maendeleo, katika Serikali ambayo itaundwa, itahusisha wanawake na viongozi wa siasa bila kujali itikadi zao,” anasema.

Anasema ili kuhakikisha kata hiyo inakuza pato lake, ataboresha soko la Sekenke ambalo kwa miaka 30 sasa, halijawahi kufanyiwa ukarabati hivyo linakabiliwa na hali mbaya ya uchafu na hakuna kiongozi anayejali.

Anaongeza kuwa, tatizo hilo limesababishwa na CCM ambayo imejibinafsisha ardhi ndani ya soko hilo hivyo kusababisha kukosekana mwekezaji wa kuliboresha ili lisaidie kuongeza pato la kata hiyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...