Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, September 17, 2010

Mrembo Julieth kuwakilisha Miss Progress Italia


Na Mwandishi Wetu
MREMBO Julieth William aliyeshika nafasi ya tatu katika mashindano ya Miss
Tanzania 2009, ameteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia ya
Miss Progress International yatakayofanyika nchini Italia Septemba 26 mwaka huu.
Mrembo huyo aliyetarajiwa kuondoka nchini jana jioni kuelekea nchini Italia kwa
ajili ya kinyang’anyiro hicho alikabidhiwa bendera jana na Mkurugenzi Mtendaji
wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Aloyce Nzuki.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa bendera, mrembo huyo alisema aliteuliwa na
waandaaji wa mashindano hayo kupitia mtandao wa mashindano ya Miss Tanzania na
kwamba Tanzania inashiriki mchuano huo kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Alisema kabla ya kushiriki watakuwa kambini kwa wiki mbili na yeye kama
mwakilishi wa Tanzania ana jukumu la kuutangaza utalii wa ndani ya nchi kupitia
Utamaduni.
“Nimefarijika kuwakilisha nchi kupitia mashindano haya kwani hii ni mara ya
kwanza kwetu kushiriki hivyo ni changamoto kubwa kwangu binafsi na nchi kwa
ujumla,” alisema.
Alisema ana imani ataiwakilisha vyema Tanzania na ushiriki wake katika
mashindano hayo utaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii na pato
la taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Nzuki alisema TTB inajivunia ushiriki wa mrembo huyo katika
mashindano hayo ya utalii ya ngazi ya kidunia kwani pamoja na mambo mengine
mrembo husika atakuwa balozi mzuri wa kazi za bodi hiyo katika kuutangaza utalii


wa ndani.
Alisema waandaaji wameifanya Tanzania iendelee kusomeka vizuri katika soko la
utalii duniani na kwamba kuchaguliwa kwa mwakilishi huyo ni kitu cha kujivunia
kwani ni nchi chache za kiafrika zinazoshiriki mashindano hayo.
Mashindano hayo ambayo yanaandaliwa na Taasisi ya Miss Progress International
ya Italia yanafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake na yanashirikisha
warembo kutoka nchi 60 tofauti duniani zikiwemo sita za Afrika ambazo ni
Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia,Algeria na Nigeria.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...