Marquee
tangazo
Thursday, September 23, 2010
Zawadi Rock City Marathon hadharani
Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya sh. mil 5/- zitatolewa kama zawadi za fedha taslimu katika mashindano ya riadha ya kilomita 21yanayojulikana kama ‘Rock City Marathon 2010’ yatakayofanyika Septemba 26 mwaka huu Jijini Mwanza.
Mratibu wa Mashindano hayo Raymond Kanyambo wa Kampuni ya Capital Plus inayoandaa mashindano hayo alisema fedha hizo ni zawadi kwa washindi 20 wa mwanzo katika aina tano za mashindano zitakazohusika katika mchuano huo.
Alisema washindi katika mbio ndefu za km 21 kwa upande wa wanaume na wanawake kila mmoja atapata sh. 500,000/- wakati washindi wa pili wataondoka na sh.300,000/-, washindi nafasi ya tatu watapata 200,000/- na nafasi ya nne wataweka kibindoni sh.100,000/-.
Alifafanua kuwa zawadi hizo zitakuwa zikipungua ambapo mshindi wa 20 atapata sh 20,000/- kama kifuta jasho na kwamba katika mbio za km 5 washindi wa kwanza watanyakua sh.100,000/- wakati watakaoshika nafasi ya pili watapata 80,000/- na nafasi ya tatu wataondoka na sh.70,000/-
Kwa mbio za km 3 kwa walemavu washindi watapata sh. 50,000/- wakati km 3 kwa watu wenye umri wa miaka 55 na zaidi washindi wataondoka na sh.30,000/- wakati washindi upande wa watoto watapatiwa medali .
Kanyambo alisema CPI kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Tanzania (RT) walifikia uamuzi wa kugawanya zawadi husika katika viwango hivyo katika kuongeza hamasa ya ushiriki tofauti na inavyokuwa katika mashindano mengi ambapo zawadi huwahusu washindi watatu wa juu pekee.
“Wigo wa zawadi kwa mashindano ya mwaka huu umepanuliwa ukilinganisha na mwaka jana na hii tumeifanya makusudi kwa kushirikiana na uongozi wa TR katika kuongeza hamasa ya ushiriki,” alisema.
Kwa upande mwingine alisema maandalizi kuelekea katika mashindano hayo yapo katika hatua nzuri ambapo karibu mambo yote yamekamilika na kwamba usajili wa kushiriki utafanyika Mwanza kuanzia Ijumaa ya Sept 24, mwaka huu.
Alivitaja vituo vitakavyohusika na usajili kuwa ni pamoja na ofisi za uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Mgahawa wa Pizeria, Isamilo Lodge,Shule ya Msingi St Marrys’ Kiteta na Shule ya Msingi Kitangiri.
Mashindano haya yamedhaminiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL),Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Kampuni ya Executive Solutions, Nyanza Bottlers Ltd, Hoteli ya New Africa, NSSF, Tigo Tanzania,Clouds FM na Isamilo Lodge ya Mwanza.
Rock City Marathon mwaka huu pamoja na mbio ndefu pia itahusisha mbio za kilomita 5 kwa wote , mbio za kilomita 3 kwa wazee wa kati ya umri wa miaka 55 na zaidi, mbio za kilomita 3 kwa watu wenye ulemavu na mbio za kilomita 2 kwa
watoto wa kati ya umri wa miaka 7 -10.
Ada za ushiriki kwa mashindano haya ni sh. 2,000/= kwa mbio zote na watoto ni bure lakini wale wataoshiriki kutoka mashuleni, shule husika zitapaswa kulipa ada ya pamoja ya sh.10,000/-
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment