KAMATI ya Ufundi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemteua Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kuwa kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ inayojiwinda na michuano ya Tusker Chalenji Cup inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Uteuzi wa Mkwasa umekuja wiki chache baada ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti wake Juma Nkamia, kumpiga ‘stop’ kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mdenish Jan Poulsen, kuifundisha timu hiyo ili kuepusha msigano baina ya Tanzania Bara na Visiwani.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema, wamezingatia ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge kutaka Poulsen abakie na jukumu la kuinoa Taifa Stars, hivyo kumteua Mkwasa kukinoa kikosi cha hicho akisaidiawa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Alisema, Kamati ya Ufundi pia imemteua Khalidi Abeid kuwa Meneja wa timu hiyo ambayo ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo ikiwa imepangwa katika kundi A pamoja na timu za Ethiopia, Rwanda na Djibouti.
Angetile, alisema, wameshindwa kutangaza ratiba ya kituo cha Mwanza ili kutoa nafasi kwa wenyeji wa kituo hicho Mkoa huo kujiandaa vya kutosha ambapo wataanika ratiba ya kundi hilo baada ya siku mbili.
No comments:
Post a Comment