Kiungo Michael Bolou Kipre wa Azam FC ameiongoza timu yake kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo jioni kwenye uwanja wa Azam Chamazi.
Azam FC imepata ushindi huo wa pili mfulilizo katika mechi zake za maandalizi ya ligi kuu na michuano ya Kombe la Mapinduzi, Azam waliifunga Yanga 2-0 kwenye mchezo wake wa kwanza wa kirafiki,
Kipre alikuwa wa kwanza kufungua kalamu hiyo ya magoli katika dakika ya 26 na dakika sita baadaye Khamis Mcha aliifungia klabu hiyo goli la pili na kupeleka timu mapumziko Azam wakiwa mbele kwa 2-0.
Katika mchezo huo uliozikutanishi timu zote zinazocheza ligi kuu ya Vodacom, JKT Ruvu walicheza katika kiwango kizuri na kufanya mchezo kuwa wa kiushindani japo walikuwa nyuma kwa idadi hiyo ya magoli.
Kiungo JKT ruvu kilikuwa chini ya mchezaji Mohamed Banka akishirikiana na wachezaji wengine wa timu hiyo huku Azam FC kulikuwa na Abdi Kassim, Mcha, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na Kipre walioweza kuichezesha timu hiyo katika kipindi chote cha kwanza.
Kipindi cha pili timu zote ziliongeza kasi na kufanya mabadiliko Azam FC walitoka golikipa Mwadini Ally, Agrey Moris, Waziri Salum, Abdulhalim Humud, Abdi, Kipre na Gaudence Mwaikimba wakaingia golikipa chipukizi Aishi Mfula aliyechukua vyema nafasi hiyo katika dakika ya 72, Luckson Kakolaki, Samir Haji, Abdulghan Gulam, Himid Mao, Zahor Pazi na John Bocco.
Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu kwa Azam na kupelekea dakika ya 78 Mcha kupachika goli la tatu baada ya kipa wa JKT Ruvu Amani Simba kupangua shuti la Bocco na mpira huo kumkuta mcha aliyeupeleka wavuni na kumaliza mchezo kwa Azam kupata ushindi huo wa 3-0.
Kocha msaidizi wa Azam, Kali Ongalah amesema ushindi wa mchezo huo ni maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi zijazo.
“Tumeshinda huu mchezo wa pili, hatujaruhusu hata goli moja hivyo upande wa ulinzi inaonyesha tupo vizuri na tukiendelea hivi tutafikia malengo yetu” alisema Kali.
Azam FC itaondoka Dar es Salaam siku ya Jumapili kuelekea Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi, watacheza mechi ya kwanza siku ya Jumatatu dhidi ya Kikwajuni FC mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Amaan.
No comments:
Post a Comment