Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akiwasalimia na kuwashukuru mamia ya
wakazi wa mji wa Dodoma mapema leo asubuhi waliojitokeza kushuhudia
maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika kwenye uwanja wa
Mashujaa, mjini Dodoma.PICHA NA MICHUZI JR-DODOMA
*Asema akishahamia,
Mawaziri na Naibu Mawaziri wote wafuatie mara moja
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atahamia
Dodoma ifikapo Septemba, mwaka huu kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria
kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumatatu, Julai 25, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na kuwashukuru kwa ushiriki wao kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa zilizofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.
“Jana nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu
ninataka kuhamia Dodoma ifikapo Septemba,” amesema na kushangiliwa na mamia ya
wakazi wa mji wa Dodoma waliohudhuria maadhimisho hayo.
Amesema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie
madarakani, kazi nyingi zimefanyika na wananchi wameziona na kwamba sasa hivi
kazi iliyobakia ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
“Wananchi kazi mmeziona na sasa tunaenda
kwenye utekelezaji. Ninatoa agizo kuwa mawaziri na manaibu wote wahame mara
moja kutoka Dar es Salaam na kuja Dodoma. Wana ofisi ndogo Dodoma na kwa kuwa
wamekuwa wakiishi wakati wote wa Bunge, wahamie mara moja. Mimi nahamia
Septemba, na utekelezaji wake nitausimamia kwa juhudi zote,” alisisitiza.
Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo
kutunza amani ya nchi na kudumisha umoja uliopo na pia akataka watumie fursa
hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na hoteli za
kitalii ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa
kuishi.
Wakati huo huo, mgeni rasmi kwenye
maadhimisho hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika
muda wa siku tatu amerudia kusisitiza nia ya Serikali kuhamia Dodoma katika kipindi chake cha uongozi ili kutekeleza
ndoto ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kutaka makao
makuu ya nchi yawe Dodoma.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa
Dodoma kwenye uwanja wa mashujaa huku akishangiliwa, Rais Magufuli amesema atahakikisha
Dodoma inakuwa makao makuu ndani ya miaka minne na miezi minne iliyobakia
kwenye awamu ya kwnza ya uongozi wake.
“Kama wabunge karibu 300 na mawaziri na
manaibu wao ambao hawafiki 30 wanakaa hapa kwa miezi mitatu na maisha
yanakwenda, kama makao makuu ya chama kinachotawala nchi yako hapa sioni sababu
ni kwa nini Serikali ninayoiongoza iendelee kubakia Dar es Salaam,” amesema.
Mara kwanza kutoa kauli hiyo, ilikuwa ni
Jumamosi iliyopita, Julai 23, 2016 wakati akitoa hotuba yake ya kwanza mara
baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkutano Mkuu
maalum wa chama hicho.
Rais Magufuli amesisitiza wananchi na wanasiasa
kutunza amani na kudumisha amani iliyokuwepo nchini. Pia amewataka Watanzania
wote kuendelea kuwaenzi mashujaa walioipigania nchi hii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JULAI 25,
2016.
No comments:
Post a Comment