Jamal Malinzi
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza
Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Katika
salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira
wa miguu Afrika, Rais Hayatou amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi
fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.
Amesema
CAF ina imani uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika mpira
wa miguu havitausaidia mpira wa miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa
ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha
zaidi vijana wa bara hili.
Rais
Hayatou amemtakia Rais Malinzi kila la kheri katika kipindi chake cha
uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko pamoja naye katika kusukuma mbele
gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.
PAMBANO LA YANGA, MGAMBO SHOOTING LAINGIZA MIL 37/-
Pambano
la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mgambo Shooting lililochezwa
jana (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh.
37,915,000.
Washabiki
waliohudhuria mechi hiyo namba 46 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na
ushindi wa mabao 3-0 walikuwa 6,515 ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000,
sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Mgawo
wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) sh. 5,783,644.07, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,145,790 wakati
kila klabu ilipata sh. 8,550,741.95.
Wamiliki
wa uwanja walipata sh. 4,347,834.89, gharama za mchezo sh.
2,608,700.93, Bodi ya Ligi sh. 2,608,700.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira
wa Miguu (FDF) sh. 1,304,350.47, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar
es Salaam (DRFA) sh. 1,014,494.81.
SIMBA, KAGERA SUGAR KUUMANA KESHO
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaanza raundi ya 12 kesho (Oktoba 31 mwaka huu
kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar itakayofanyika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Viingilio
katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kupitia TBC 1
vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.
Nayo
Yanga itashuka uwanjani Novemba Mosi mwaka huu katika mechi nyingine ya
ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Novemba
2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union
(Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa
Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na
Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
Raundi
hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City
itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.
Mechi
za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7
mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs
Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania
Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)