Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, October 31, 2013

RAIS WA CAF AMPONGEZA MALINZI


Jamal Malinzi
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Katika salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira wa miguu Afrika, Rais Hayatou amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.
Amesema CAF ina imani uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika mpira wa miguu havitausaidia mpira wa miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha zaidi vijana wa bara hili.
Rais Hayatou amemtakia Rais Malinzi kila la kheri katika kipindi chake cha uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko pamoja naye katika kusukuma mbele gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.
PAMBANO LA YANGA, MGAMBO SHOOTING LAINGIZA MIL 37/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mgambo Shooting lililochezwa jana (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 37,915,000.
Washabiki waliohudhuria mechi hiyo namba 46 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 walikuwa 6,515 ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 5,783,644.07, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,145,790 wakati kila klabu ilipata sh. 8,550,741.95.
Wamiliki wa uwanja walipata sh. 4,347,834.89, gharama za mchezo sh. 2,608,700.93, Bodi ya Ligi sh. 2,608,700.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,304,350.47, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,014,494.81.
SIMBA, KAGERA SUGAR KUUMANA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaanza raundi ya 12 kesho (Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Viingilio katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kupitia TBC 1 vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.
Nayo Yanga itashuka uwanjani Novemba Mosi mwaka huu katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...